Morocco haitakuwa tena mwenyeji wa mechi ya fainali ya Kombe la Dunia la FIFA kwa mwaka 2030 kufuatia matukio yaliyojitokeza wakati wa fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 yaliyohusishwa na changamoto za usalama na usimamizi wa mashindano.
Hivyo kombe la Dunia la 2030 linatarajiwa kuandaliwa kwa pamoja na Uhispania, Ureno na Morocco, ambapo awali Morocco ilikuwa katika kinyang’anyiro cha kupewa heshima ya kuandaa mechi ya fainali ya michuano hiyo mikubwa zaidi duniani.
Hata hivyo mizozo na matukio ya vurugu yaliyoripotiwa wakati wa fainali ya AFCON 2025 kati ya wenyeji Morocco na Senegal yameonekana kuzua wasiwasi mkubwa kuhusu uwezo wa nchi hiyo katika kudhibiti usalama na usimamizi wa matukio makubwa ya kimataifa.
Akithibitisha mabadiliko hayo Rafael Louzán, Rais wa Shirikisho la Soka la Uhispania (RFEF), amesema kuwa Uhispania sasa imekabidhiwa rasmi jukumu la kuandaa mechi ya fainali ya Kombe la Dunia 2030, uamuzi uliofikiwa baada ya tathmini ya kina ya maandalizi na masuala ya kiusalama.
Aidha amuzi huo unaashiria pigo kwa ndoto ya Morocco kuandaa fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza, huku Uhispania ikiongeza hadhi yake kama mmoja wa waandaaji wakuu wa mashindano hayo ya kihistoria.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime