JKT Tanzania Yaongoza Ligi kuu kwa Kadi Nyingi za Njano

Wakati ikiendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, timu ya JKT Tanzania imeibuka pia kuwa kinara wa kupata kadi nyingi za njano mpaka sasa msimu huu.

Maafande hao wanaongoza ligi wakiwa na pointi 17, lakini pia wamekusanya kadi 22 za njano katika michezo 10 waliyocheza. Hali hiyo ni tofauti kabisa na Yanga, ambayo licha ya kuwa miongoni mwa timu bora, imepata kadi moja tu ya njano.

Mbali na hilo JKT Tanzania ndiyo timu yenye sare nyingi zaidi ligi kuu ikiwa nazo tano, huku pia ikiwa miongoni mwa timu zenye mabao mengi ya kufunga, ikifunga jumla ya mabao 12, sawa na Yanga.

Kwa mujibu wa takwimu za michezo kutoka Dawati la Nipashe, timu inayoshika nafasi ya pili kwa kupata kadi nyingi za njano ni Namungo, iliyokusanya kadi 14 katika michezo nane. Nafasi ya tatu inashikiliwa na Dodoma Jiji yenye kadi 13 baada ya kucheza michezo nane.

Nafasi ya nne inashikiliwa kwa pamoja na Fountain Gate na TRA United, kila moja ikiwa na kadi 11 za njano. Hata hivyo, Fountain Gate imecheza michezo 10, wakati TRA United imeshuka dimbani mara saba pekee.

Kwa nafasi ya tano, kuna Mashujaa FC yenye kadi 10 baada ya michezo tisa, sambamba na Mbeya City iliyopata kadi hizo hizo baada ya michezo 10, pamoja na Prisons ambayo imecheza michezo saba.

Timu nyingine ni Mtibwa Sugar yenye kadi tisa katika michezo minane, huku Pamba Jiji na KMC kila moja ikipata kadi nane baada ya michezo tisa. Coastal Union ina kadi saba baada ya michezo minane.

Kwa upande mwingine, Singida Black Stars na Azam FC kila moja imepata kadi tano katika michezo mitano, wakati Simba SC imeonyeshwa kadi nne katika idadi hiyo hiyo ya michezo.

Aidha miongoni mwa timu iliyopata kadi chache zaidi mpaka sasa ni Yanga, ambayo imeonyeshwa kadi moja tu ya njano katika michezo sita iliyocheza, jambo linaloonesha nidhamu ya hali ya juu ndani ya uwanja.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii