WIZARA YA MADINI YAZITAKA KAMPUNI ZA KIGENI KUHESHIMU SHERIA, YAWAHAMASISHA WATANZANIA KUCHANGAMKIA FURSA MIGODINI.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ameziagiza kampuni kubwa za kigeni zinazowekeza katika sekta ya madini nchini kuzingatia kikamilifu sheria, kanuni na masharti ya mikataba ya uwekezaji ili kuhakikisha Watanzania wananufaika zaidi na rasilimali za madini.

Akifungua Jukwaa la Tano la Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini lililofanyika jijini Mwanza, Mavunde alisema Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Sheria ya Madini pamoja na Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania za mwaka 2018, huku ikisisitiza kampuni za madini kutoa kipaumbele kwa ajira, mafunzo, uhawilishaji wa teknolojia na ununuzi wa bidhaa pamoja na huduma kutoka kwa Watanzania.

Waziri Mavunde aliwahimiza Watanzania, hususan wajasiriamali na kampuni za ndani, kuungana na kujijengea uwezo wa kitaalamu na kiusimamizi ili kushindana katika zabuni za migodini na kutumia kikamilifu fursa zilizopo badala ya kuziacha zinufaishwe na kampuni za nje pekee.


Alisema maboresho ya sera na sheria za madini yaliyofanyika tangu mwaka 2017 yameongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa. Alibainisha kuwa mapato yasiyo ya kikodi ya sekta ya madini yameongezeka kutoka takribani shilingi bilioni 116 mwaka 2015/2016 hadi zaidi ya shilingi trilioni 1.3 kufikia Juni 30, 2026, kutokana na kuimarishwa kwa usimamizi wa sekta hiyo, kuanzishwa kwa masoko ya madini na kudhibiti biashara haramu ya madini.


Kwa mujibu wa Waziri huyo, mwaka 2025 migodi mikubwa na ya kati ilizalisha ajira rasmi 20,421, ambapo ajira 19,695 sawa na asilimia 96.4 zilitolewa kwa Watanzania, hatua inayodhihirisha kuongezeka kwa ushiriki wa wazawa katika sekta hiyo.

Aidha, alisema manunuzi ya bidhaa na huduma yaliyofanywa na migodi mwaka 2025 yalifikia shilingi trilioni 5.35, huku kampuni za Kitanzania zikifanya biashara yenye thamani ya shilingi trilioni 4.60, sawa na asilimia 86 ya manunuzi yote.

Mavunde pia alitoa rai kwa taasisi za fedha kuweka mazingira rafiki ya utoaji wa mikopo kwa Watanzania na kampuni za ndani ili ziweze kuanzisha viwanda vya kuzalisha bidhaa zinazohitajika migodini, hatua itakayopunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje na kuongeza thamani ya madini nchini.


Hata hivyo, Waziri huyo alieleza kuwa bado zipo changamoto ikiwemo baadhi ya kampuni za kigeni kutotekeleza kikamilifu matakwa ya sheria, pamoja na baadhi ya kampuni za Kitanzania kushindwa kutimiza viwango vya mikataba au kuweka bei zisizoendana na soko. Alisisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayekiuka Sheria ya Madini na Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dk Janet Lekashingo amesema utekelezaji wa sera ya ushirikishwaji wa wazawa umeendelea kuimarika, akibainisha kuwa idadi ya kampuni zilizowasilisha mipango ya ushirikishwaji imeongezeka kutoka 51 mwaka 2018 hadi 1,312 mwaka 2025. 


Naye Meneja wa Rasilimali Watu wa Geita Gold Mining Limited (GGML), Dominick Marandu amesema asilimia 98 ya wafanyakazi zaidi ya 7,000 wa mgodi huo ni Watanzania, huku asilimia 97 ya manunuzi yaliyofanyika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2026 yakitoka kwa kampuni za wazawa.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii