Yanga Yatwaa Tuzo Mbili za Desemba

KLABU ya Young Africans (Yanga) imeendelea kung’ara katika Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kutwaa tuzo mbili za mwezi Desemba 2025, ambazo ni Kocha Bora na Mchezaji Bora wa mwezi.

Kiungo wa Yanga, Duke Abuya, ametangazwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Desemba 2025 baada ya kuonyesha kiwango cha juu katika michezo aliyocheza mwezi huo.

Abuya aliisaidia Yanga kushinda mechi zote mbili alizocheza, huku akihusika moja kwa moja katika mabao mawili ndani ya dakika 180, jambo lililompa nafasi ya kuwashinda Nassor Saadun wa Azam FC na Prince Dube wa Yanga waliokuwa fainali katika tuzo hizo.

Tuzo hizo ziliandaliwa na Kamati ya Tuzo za Mwezi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Kwa upande wa benchi la ufundi, Pedro Concalves ametwaa tuzo ya Kocha Bora wa mwezi Desemba baada ya kuiongoza Yanga kushinda michezo miwili muhimu na kupanda kutoka nafasi ya nne hadi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Concalves aliwashinda makocha Florent Ibenge wa Azam FC na Etienne Ndairagije wa TRA United waliokuwa wakishindania tuzo hiyo.

Mafanikio hayo yanaendelea kuimarisha ubora wa Yanga katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2025/2026.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii