Achraf Hakimi kupanda kizimbani kwa tuhuma za ubakaji

Beki wa klabu ya Ufaransa, Paris Saint-Germain na timu ya taifa ya Morocco, Achraf Hakimi, ameshtakiwa rasmi kwa tuhuma za kumbaka mwanamke mmoja, wakili wake na mwendesha mashtaka wa Ufaransa wamethibitisha.

Mwezi Februari mwaka 2023, mwanamke mmoja aliyekuwa na umri wa miaka 24, aliwaambia polisi katika eneo la Val-De-Marne kusini-mashariki mwa Paris kwamba Hakimi alikuwa amembaka.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Morocco mwenye umri wa miaka 27, ambaye alikuwa na mchango mkubwa kwa timu yake ya taifa ya Morocco na hata kuisaidia kuwa timu ya kwanza ya Kiafrika kufuzu nusu fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2022, amekanusha tuhuma dhidi yake.

"Ninasubiri kesi hii kwa utulivu, ambayo itaruhusu ukweli kufichuka hadharani." Alisema Hakimi kwenye ukurasa wa kijamii wa X.

Wakili wa Hakimi, Fanny Colin, alisema kesi imeamriwa na mwendesha mashtaka katika kitongoji cha Nanterre cha Paris.

Mlalamikaji alisema alikutana na Hakimi mnamo Januari mwaka 2023 kwenye Instagram na akaenda nyumbani kwake kwa teksi iliyokodiwa na mchezaji huyo, chanzo cha polisi kilisema.

Aidha alidai kwamba mchezaji huyo alimbusu, akamgusa bila idhini yake kisha akambaka.

Hata hivyo amesema aliweza kumsukuma na kumtumia ujumbe rafiki yake, ambaye alikuja kumchukua.

Kocha wa PSG Luis Enrique, alipoulizwa kuhusu hilo katika mkutano na waandishi wa habari kuelekea ya mchujo ya Ligi ya mabingwa dhidi ya Monaco, alisema: "Jambo hili liko mikononi mwa mamlaka."

Wakili wa mlalamikaji, Rachel-Flore Pardo, amesema mteja wake alifurahi kusikia kwamba kesi hiyo ilikuwa inaenda mahakamani, akidai mahakama imekuwa mfano mzuri katika kushughulikia kesi hiyo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii