Tetemeko La Liga: Sergio Ramos Ajiandaa Kuinunua Sevilla

Kwa mujibu wa ripoti ya Cadena SER gwiji wa soka wa Hispania, Sergio Ramos, amefikia makubaliano ya kimsingi na wanahisa wa klabu ya Sevilla FC kuhusu ununuzi wa klabu hiyo.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa pande zote zimekubaliana kwa hatua ya awali, huku mchakato wa kuchambua hali ya kifedha ya klabu ukiendelea kabla ya kufikia makubaliano ya mwisho.

“Sergio Ramos na wanahisa wa klabu hiyo wamefikia makubaliano ya kimsingi, na sasa watafanya tathmini ya kina ya hali ya kifedha ili kufikia makubaliano ya mwisho,” imeeleza sehemu ya ripoti hiyo.

Aidha, Cadena SER imesisitiza kuwa uchambuzi wa kina wa hesabu na madeni ya klabu ni hatua muhimu kabla ya kukamilisha mchakato huo wa ununuzi.

Hatua hiyo inaelezwa kuwa ya kihistoria kwa Sergio Ramos, ambaye baada ya mafanikio makubwa ndani ya uwanja wa soka kama mchezaji, sasa anaelekea kuingia katika usimamizi na umiliki wa klabu, hatua itakayomuweka katika ngazi ya juu ya uongozi wa soka la kimataifa.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii