Tume huru ya kuchunguza vurugu za Oktoba 29, 2025, iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imeagiza vyombo vya habari nchini Tanzania kutotoa moja kwa moja ushahidi au taarifa zinazotolewa na waathirika wa ghasia zilizotokea wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.
Uamuzi huo, ulioangaziwa katika taarifa ya Januari 24 mwaka huu umetolewa kwa lengo la kulinda usalama, faragha, na afya ya akili ya waathirika ambapo tume hiyo inayoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman na kaimu wake Jaji Mstaafu Ibrahim Juma, imesema hatua hiyo ilichukuliwa baada ya kero kuibuka kuwa taarifa binafsi za waathirika zinasambazwa mitandaoni bila idhini yao.
“Taarifa binafsi zinazochapishwa zinaweza kuwatesa waathirika, kusababisha msongo wa mawazo na changamoto ndani ya familia zao,” alisema Profesa Juma.
Hata hivyo, uamuzi huo umepokelewa kwa mtazamo mchanganyiko kutoka kwa wadau wa habari na wataalamu wa afya ya akili. Kajubi Mukajanga, mchambuzi wa masuala ya habari, amesema:
“Sijui kwa nini wamechukua uamuzi huo, kwa sababu mambo yaliyotokea kipindi kile yalikuwa hadharani. Watu waliaona na kuyajadili.”
Kwa upande wake, Saldine Kimangale, mtaalamu wa afya ya akili, ameongeza kuwa:
“Sio wanahabari pekee, hata mazungumzo ya kawaida yanaweza kufufua kumbukumbu za tukio lililotokea, si lazima iwe ripoti ya habari.”
Hata hivyo tume hiyo tayari imeshakamilisha kusikiliza waathirika katika wilaya za Kinondoni, Temeke, Ilala, na Ubungo mkoani Dar es Salaam na inaendelea na mikutano katika mikoa ya Dodoma, Shinyanga, Ruvuma, na Iringa, ikiwa na lengo la kukusanya taarifa za matukio yote yaliyojitokeza wakati na baada ya uchaguzi.
Aidha vurugu hizo, zilizofuatana na maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi, zimesababisha mamia kufariki, huku Rais Samia Suluhu Hassan akitangazwa mshindi wa uchaguzi huo.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime