Jeshi la Polisi Lachunguza Kifo cha Mwanaume Ndani ya Nyumba ya Kulala Wageni Morogoro

Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linaendelea na uchunguzi wa tukio la kifo cha Gidion Ebenezeri Mbwambo (34) kilichotokea leo Januari 27 mwaka huu katika nyumba ya kulala wageni maarufu kwa jina la Kisanga, iliyopo mtaa wa Nguzo, kata ya Mazimbu, Manispaa ya Morogoro.

Kwa mujibu wa taarifa za awali marehemu alikutwa amefariki ndani ya chumba namba 106 alichokuwa amepanga baada ya watu waliokuwapo kubaini michirizi ya damu na maji ikitoka nje ya mlango wa chumba hicho.

Baada ya mlango kuvunjwa ilibainika kuwa marehemu alikuwa amefariki dunia huku akiwa na jeraha la kujikata koromeo la shingo kwa kutumia kitu chenye makali na mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani.

Uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa marehemu alijitoa uhai kwa kutumia kitu chenye makali akiwa katika hali ya ulevi, huku uchunguzi wa kina ukiendelea ili kubaini mazingira kamili ya tukio hilo.

Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wamiliki wa nyumba za kulala wageni kuzingatia na kufuata taratibu zote za kisheria katika kuwatambua na kuhifadhi taarifa sahihi za wageni wanaolala katika maeneo yao.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii