Utata Wazuka Juu ya Kifo cha Diwani Nyamugali, ACT-Wazalendo na Polisi Watofautiana

Utata umeibuka kufuatia kifo cha Diwani wa Kata ya Nyamugali Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe Majaliwa Abbas Hamis baada ya chama chake cha ACT-Wazalendo kutilia shaka chanzo cha kifo hicho huku Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma likisisitiza kuwa kimesababishwa na ajali ya pikipiki.

Kupitia taarifa iliyotolewa katika ukurasa rasmi wa Instagram wa ACT-Wazalendo chama hicho kimeeleza kuwa mazingira yanayozunguka kifo cha diwani huyo yanatia shaka.

Kwa mujibu wa chama hicho mwili wa marehemu haukuwa na majeraha yanayoashiria ajali ya barabarani huku koti lake likidaiwa kukutwa pembeni ya mwili.

Aidha chama hicho kimesema simu ya marehemu haikuwa na laini na shingoni kulionekana alama zinazofanana na kunyongwa kutokana na hali hiyo, ACT-Wazalendo kimetaka kufanyika kwa uchunguzi huru na wa kina ili kubaini chanzo halisi cha kifo hicho.

Kwa upande wao Polisi Mkoa wa Kigoma wamesema uchunguzi wao wa awali unaonesha kuwa marehemu alifariki kutokana na ajali ya barabarani iliyotokea Januari 23 mwaka huu majira ya saa nne usiku katika Kijiji cha Songambele.

Polisi wamesema marehemu alikuwa akiendesha pikipiki aina ya Kinglion yenye namba MC 709 BCW akiwa amebeba mzigo wa mahindi, ndipo aligongwa na gari lisilofahamika na kufariki dunia papo hapo.

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa taratibu zote za kiuchunguzi zilifanyika eneo la tukio vielelezo vilikusanywa, na simu ya marehemu ilitumika katika kusaidia kutambua utambulisho wake ambapo polisi wameendelea kusisitiza kuwa kifo hicho kilitokana na ajali kinyume na madai yanayotolewa na ACT-Wazalendo.

   


#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii