Rais Samia Aadhimisha Siku ya Kuzaliwa kwa Kupanda Miti Zanzibar

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema amechagua kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa kwa kupanda miti kama sehemu ya kutimiza wajibu wake wa kulinda na kuhifadhi sayari ya dunia, pamoja na kuacha urithi kwa vizazi vijavyo.

Dk. Samia ametoa kauli hiyo leo Jumanne Januari 27, 2026, wakati wa hafla ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa iliyofanyika katika Bungi Kilimo Kizimkazi, Zanzibar, hafla iliyojumuisha upandaji miti na kukata keki.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Samia amesema kuwa Watanzania wa kizazi cha sasa walirithi uoto wa asili na mazingira yaliyo bora zaidi, hali ambayo imebadilika kwa kiasi kikubwa kwa sasa.

“Sisi tulirithi uoto wa asili mwingi sana. Tulirithi nchi yetu ambayo haikuwa imeharibiwa kiasi hiki. Tulirithi miti mingi ya matunda, mingine shambani na mingine kujiotea,” amesema Rais Samia.

Ameongeza kuwa hali ya sasa imebadilika kiasi kwamba watoto wengi hulazimika kununua matunda sokoni, tofauti na zamani ambapo yalipatikana kwa urahisi kutoka porini.

“Leo mtoto wetu akitaka kula pera lazima akanunue sokoni, wakati sisi tulikuwa tunapita msituni na kula mapera ya aina yoyote tunayoyataka,” ameongeza.

Kwa mujibu wa Rais Samia, kupotea kwa miti hiyo ni changamoto inayohitaji juhudi za pamoja, akisisitiza kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kushiriki kurejesha uoto wa asili na miti ya asili ili kuacha urithi bora kwa watoto wa sasa na wa baadaye.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kumpa afya njema na fursa ya kuiona tena tarehe 27 Januari, huku akiwatakia heri Watanzania wote wanaosherehekea siku yao ya kuzaliwa tarehe hiyo.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii