Siku ya Jumatano, Januari 21, katika Jukwaa la Uchumi Duniani huko Davos, na kisha siku iliyotangulia katika Ikulu ya White House, katika kumbukumbu ya miaka ya kwanza ya kurudi kwake madarakani, Rais wa Marekani Donald Trump ameendelea na mashambulizi yake makali ya maneno dhidi ya Somalia na jamii ya Wasomali wanaoishi Marekani.
Rais wa Marekani amemlenga mbunge Ilhan Omar, mwanachama wa Chama cha Democratic mwenye asili ya Somalia ambaye amekuwa akilengwa mara kwa mara na rais huyo ktoka chama cha Republican.
Shambulio jingine kutoka kwa Donald Trump. Wakati huu, rais wa Marekani ameilenga Somalia, akiwaita wahamiaji wa Somalia "wasio na akili nyingi," akisema kwamba "Somalia si nchi," au, ikiwa ni nchi, basi ni "mbaya zaidi duniani," akiongeza kwamba "haina serikali, hakuna taasisi."
Rais pia alimkosoa mbunge Ilhan Omar, Mdemokrat kutoka Minnesota na mwanachama wa cha mrengo wa kushoto "Squad" katika Bunge, kuhusu utajiri wake wa mamilioni ya dola wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House siku ya Jumanne alasiri. Akiwa amepewa jina la "mtu asiye mwaminifu," "fisadi," na mtu ambaye "hajawahi kufanya kazi hata siku moja maishani mwake," Ilhan Omar ni lengo la kisasi cha kweli kutoka kwa rais wa Marekani. Mara kadhaa, amemsihi "kurudi Somalia," akimwita "taka," aakiongeza matusi, na kwa upana zaidi akawalenga Wasomali na Wamarekani wenye asili ya Somalia, ambao anabaini wanapaswa "kurudi walikotoka."
Mashambulizi haya ya mara kwa mara yamemfanya Ilhan Omar hivi karibuni kuelezea mtazamo wa rais kwake kama "fikra inayotia wasiwasi." Akiwa na umri wa miaka 43, mbunge huyo anawakilisha, machoni pa Donald Trump, kila kitu anachopinga kisiasa: mwanamke, Mwislamu, mhamiaji, na mwenye asili ya Kiafrika.
Ilhan Omar amejibu mara kwa mara mashambulizi ya rais, akishutumu sera ya "ubaguzi wa rangi, ubaguzi dhidi ya wageni, na chuki". Amepinga vizuizi vya visa na kuitetea jamii ya Wasomali, idadi kubwa ya watu huko Minnesota, ambapo yeye ni mwakilishi aliyechaguliwa, na lengo la mashambulizi anayoyaelezea kama "ya kuchukiza, yasiyo ya haki, na yanayodhalilisha utu."
Ilhan Omar ambaye amezaliwa Mogadishu, aliwasili Marekani akiwa na umri wa miaka 12 na familia yake, wakiishi Minnesota. Alipata uraia wa Marekani akiwa kijana, kabla ya kuchaguliwa kuwa mbunge mwaka wa 2018—mmoja wa wanawake wawili wa kwanza Waislamu waliochaguliwa—ambapo anatetea nafasi za kimaendeleo.
Hii si mara ya kwanza Donald Trump kushambulia Somalia hadharani. Mnamo Januari 13, serikali ya Marekani ilitangaza kuondoa hadhi ya kuwalinda wahamiaji wa Somalia kutokana na kufukuzwa nchini. Uamuzi huu ni sehemu ya kampeni pana inayoendeshwa na utawala wa Rais Donald Trump dhidi ya jamii ya Wasomali—kubwa zaidi nchini Marekani ikiwa na watu 80,000—ambao wanalengwa hasa katika jimbo la Minnesota.
Mnamo mwezi Desemba 2025, alitangaza nia yake ya "kusitisha kabisa uhamiaji kutoka nchi zote za Dunia ya Tatu," akisema kwamba hataki tena kukaribisha, kwa maneno yake, "kuingia uchafu nchini mwetu."
Sambamba na ugumu huu wa sera za uhamiaji, utawala wa Trump uliongeza ushiriki wake wa kijeshi nchini Somalia. Tangu kurudi madarakani, zaidi ya mashambulizi 125 ya angani yamefanywa nchini Somalia, idadi ikizidi jumla ya mashamblizi yaliyofanywa chini ya utawala wa George W. Bush, Barack Obama, na Joe Biden. Mashambulizi haya yanalenga hasa Al Shabab, mshirika wa Al Qaeda ambayo imekuwa akiendesha uasi dhidi ya taifa la Somalia kwa zaidi ya miaka ishirini.