Uhaba wa makipa bora unaoonekana katika soka la Tanzania kwa sasa umetajwa kuchangiwa na kukosekana kwa mafunzo sahihi ya kitaalamu, kuvunjika kwa misingi ya maendeleo ya wachezaji pamoja na tabia ya baadhi ya makipa wa kisasa kudharau ushauri wa makipa wakongwe waliowahi kulinda lango.
Kauli hiyo imetolewa na aliyekuwa golikipa wa Timu ya Taifa (Taifa Stars) na klabu ya Yanga na Pan African, Juma Pondamali, katika mazungumzo maalum na vyombo vya haabari ambapo amedai kuwa miongoni mwa makipa walioweka historia ya kuifikisha Tanzania katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa mara ya kwanza mwaka 1980 nchini Nigeria.
Kwa mujibu wa Pondamali, tofauti kubwa kati ya makipa wa zamani na wa sasa ipo kwenye misingi ya mafunzo, nidhamu ya kujifunza na mchakato mzima wa ukuaji wa mchezaji.
“Tatizo kubwa la leo si kwamba hatuna makipa kabisa, wapo makipa wazuri, lakini siyo wengi. Zamani kila timu ya Ligi Kuu ilikuwa na kipa mmoja au wawili waliokuwa bora sana kiasi kwamba ilikuwa vigumu kumtofautisha namba moja na namba mbili,” alisema.
Akikumbuka enzi hizo, Pondamali alitaja ushindani mkubwa uliokuwepo miongoni mwa makipa wa vilabu mbalimbali, hali iliyoongeza ubora na hadhi ya nafasi ya golikipa.
“CDA Dodoma walikuwapo Mkala Maulid na Dan Poka; Pamba walikuwapo Madata Lubigisa na Paul Rwechungura; Pan African tulikuwapo mimi na Ally Yusuph.
“Yanga walikuwa na Joseph Fungo na Hamisi Kinye; Nyota Nyekundu Morris Nyuchi na John Bosco; Coastal Union Mohamed Mwameja na Hamisi Makene. Huwezi kujua nani namba moja au mbili,” alisema.
Alisema hali hiyo ni tofauti kabisa na ilivyo sasa, ambapo baadhi ya makipa wanaingia Ligi Kuu moja kwa moja kutoka soka la mitaani bila kupitia ngazi stahiki za maendeleo.
Pondamali, maarufu kwa jina la utani ‘Mensah’ kutokana na uwezo wake mkubwa wa kudaka, alisema makipa wengi wa sasa hawana maarifa ya msingi ya kukaa langoni.
“Makipa wengi wa sasa hawajui namna sahihi ya kukaa langoni wala lini unatakiwa utoke kupunguza lango. Lango lina njia nne, na kipa mzuri lazima azijue zote,” alisema.
Alifafanua kuwa lango lina viboksi vinne vya msingi vinavyomsaidia kipa kujipanga kulingana na mkao wa mshambuliaji.
“Unatakiwa ujue unasimama boksi gani kulingana na mpinzani alipo. Ukikosea, umefungwa. Haya ni mafunzo ya darasani,” alisisitiza.
Akisimulia safari yake binafsi, Pondamali alisema alianza kucheza soka akiwa na umri wa miaka 13 katika kikosi cha vijana cha Yanga chini ya kocha Victor Stanculescu, raia wa Romania.
“Nilipata misingi mizuri sana. Kuwapo kwenye timu za vijana zilizosimamiwa na makocha wakubwa ni njia sahihi ya kuandaa wachezaji imara,” alisema.
Pondamali alikuwa langoni wakati Taifa Stars ilipotoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Zambia mwaka 1979, matokeo yaliyoiwezesha Tanzania kufuzu AFCON 1980 kwa jumla ya mabao 2-1.
Akizungumzia mabadiliko ya soka la kisasa, Pondamali alisema mpira wa leo ni wa kisayansi zaidi kuliko zamani.
“Mpira wa sasa ni sayansi. Kuna walimu wa viungo, saikolojia, takwimu na video. Ndiyo maana mafunzo sahihi ni muhimu,” alisema.
Aliongeza kuwa hata mkao wa kipa unapopokea mpira ni sehemu ya sayansi hiyo.
“Unatakiwa kusimama juu ya vidole kama mwanariadha, si miguu yote chini, ili uwe mwepesi wa kuruka,” alifafanua.
Pondamali alipinga wazo la kuwazuia makipa wa kigeni kucheza Ligi Kuu Tanzania kwa lengo la kulinda nafasi za wazawa.
“Taifa Stars inahitaji makipa bora, siyo bora makipa. Ukizuia wageni, tutabaki na makipa wa kucheza tu, si wa kiwango cha juu,” alisema.
Ambapo alisisitiza kuwa suluhisho la msingi ni kuwekeza kwenye mafunzo bora ya makipa wazawa.
Akitolea mfano alipokuwa kocha wa makipa wa Yanga, Pondamali alisema aliwasaidia Ally Mustapha ‘Barthez’ na Deogratius Munishi ‘Dida’ kufikia kiwango cha juu sana.
Hata hivyo, alisema baadhi ya makipa wa sasa hudharau ushauri wa wakongwe.
“Sisi tupo, tumesoma ufundishaji wa kisasa, tuna vifaa na video za mafunzo. Mpira ni kujifunza kila siku mpaka unastaafu,” alionya.
Alimalizia kwa kusema kuwa endapo kutakuwa na ushirikiano kati ya makipa wa sasa na wakongwe, Tanzania inaweza kurejesha heshima yake ya kuwa na walinzi bora wa lango.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime