Simba Yatua Tunisia, Yajinasibu Kuzaliwa Upya

Klabu za Simba na Yanga zinaendelea na maandalizi ya michezo ya raundi ya tatu ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Simba ikitangaza kuzaliwa upya baada ya usajili mpya, na Yanga ikisisitiza kwenda kushambulia ugenini.

Kikosi cha Simba kimewasili salama nchini Tunisia kwa ajili ya mchezo wa raundi ya tatu ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Esperance de Tunis, utakaochezwa keshokutwa saa 1:00 usiku kwa saa za Tanzania.

Uongozi wa Simba umetangaza kuwa timu hiyo “imezaliwa upya” baada ya kukamilisha usajili wa wachezaji wanne wapya katika dirisha dogo la usajili. Wachezaji hao ni Nickson Kibabage, Ismael Toure, kipa Djibrille Kessah pamoja na kiungo wa kimataifa wa Zambia, Clatous Chama.

“Timu yetu imezaliwa upya, tumezingatia mapendekezo ya benchi la ufundi na wachezaji tuliowasajili ni wa daraja la juu na wako tayari kwa mapambano''

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema wachezaji wote wapya tayari wamejiunga na kikosi na wanatarajiwa kuwa sehemu ya timu itakayocheza dhidi ya Esperance.

Kwa upande wake, Clatous Chama amesema kurejea Simba ni kurejea nyumbani na anafahamu vyema matarajio ya klabu hiyo.

“Nimerejea Simba, ninajua nini Simba inataka.”

Wakati Simba ikiwa Tunisia, watani zao wa jadi Yanga wako nchini Misri ambapo Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves, amesema timu yake haitaenda kucheza kwa kujilinda dhidi ya Al Ahly, bali itacheza soka la kushambulia katika mchezo wa raundi ya tatu wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa kesho saa 1:00 usiku kwa saa za Tanzania.

“Hatutabadilisha aina yetu ya uchezaji. Tunakwenda kushambulia na kutafuta ushindi, licha ya kucheza na timu kubwa kama Al Ahly.”

Goncalves amesema licha ya Al Ahly kuwa klabu kubwa na yenye historia barani Afrika, Yanga inakwenda ikiwa na kujiamini na morali ya juu.

Watani hao wa jadi jana alfajiri walikutana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Yanga ikielekea Misri, huku Simba ikisafiri kwenda Tunisia.

Na hiyo ndiyo hali ya maandalizi ya Simba na Yanga kuelekea michezo ya raundi ya tatu ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii