Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Uganda, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, amethibitisha kuwa kwa sasa yuko mafichoni akihofia usalama wa maisha yake, huku hali ya kisiasa nchini humo ikiendelea kuwa tete.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Shirika la Habari la Ufaransa (AFP), Bobi Wine amesema anahifadhiwa na raia wa kawaida katika maeneo yasiyojulikana, akieleza kuwa mazingira ya usalama si salama kwake kufahamika alipo. Kauli hiyo imekuja wakati kiongozi mkongwe wa upinzani, Dkt. Kizza Besigye, akiendelea kuzuiliwa gerezani katika hali inayodaiwa kuwa mbaya kiafya.
Bobi Wine, ambaye amekuwa akikabiliwa na ukandamizaji mkubwa tangu uchaguzi wa mwaka 2021, amesema kuwa licha ya yeye kuwa mafichoni, familia yake imewekwa chini ya kizuizi cha nyumbani kwa zaidi ya wiki moja, ikizuiwa kutoka nje au kuwasiliana na watu wa nje.
Hali hiyo inatajwa kuhusishwa na shinikizo kubwa kutoka kwa utawala wa Rais Yoweri Museveni pamoja na mwanawe, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, Mkuu wa Majeshi ya Uganda (UPDF). Taarifa zinaeleza kuwa uhasama kati ya serikali na wapinzani umezidi kuongezeka, hasa baada ya Jenerali Muhoozi (miaka 51), ambaye hutajwa kama mrithi wa urais, kutoa vitisho vya wazi dhidi ya Bobi Wine.
Serikali ya Uganda imekuwa ikiwasawiri viongozi wa upinzani kama “magaidi,” hatua ambayo wachambuzi wa siasa wanaonya kuwa inaweza kutumiwa kuhalalisha matumizi makubwa ya nguvu za kijeshi dhidi yao.
Wakati huo huo, uchaguzi wa Januari 15, 2026, uliompa Rais Museveni ushindi wa muhula wa saba, unaendelea kupingwa vikali na vyama vya upinzani pamoja na waangalizi wa kimataifa, wakidai kuwa uligubikwa na udanganyifu, vitisho na matumizi ya vyombo vya dola.
Hadi sasa, hali ya usalama na mustakabali wa demokrasia nchini Uganda vinaendelea kuwa gumzo kubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na jumuiya ya kimataifa.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime