Kiongozi wa utawala wa kijeshi nchini Guinea-Bissau, Jenerali Horta N'Tam, ametangaza Desemba 6 kama tarehe ya uchaguzi wa urais na wa wabunge unaokusudiwa kuashiria madaraka kurejea kwa raia, kulingana na agizo lililosomwa kwa vyombo vya habari siku ya Jumatano, Januari 21.
Kulingana na agizo hilo, "masharti yote ya kufanyika uchaguzi huru, wa haki, na wa uwazi yametimizwa." Uchaguzi huu unatarajiwa kufanyika bila kiongozi wa utawala wa kijeshi, kulingana na hati ya mpito iliyochapishwa mapema mwezi Desemba na viongozi wa mapinduzi, hati inayotumika kama mfumo wa kisheria katika kipindi hiki kinachokusudiwa kudumu mwaka mmoja.
Miezi miwili tu baada ya mapinduzi ya Novemba 26, wakati matokeo rasmi ya chaguzi mbili (wa wabunge na wa urais) uliofanyika siku tatu mapema yakikaribia kutangazwa, Meja Jenerali Horta N’Tam, ambaye sasa ni rais wa mpito wa Guinea-Bissau, alitangaza hadharani tarehe za uchaguzi ujao.
Mnamo Januari 10, 2026, Julius Maada Bio, rais wa Sierra Leone, ambayo inashikilia urais wa mzunguko wa ECOWAS, na mwenzake wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye, walijadiliana na utawala wa kijeshi ratiba ya mpito wa kisiasa na uwezekano wa kuachiliwa huru kwa wafungwa wa maoni. Wapatanishi walitetea mpito mfupi na wa uwazi ili kurejesha utulivu wa kikatiba haraka iwezekanavyo.
Umaro Sissoco Embalo, mkuu wa nchi aliyetimuliwa na mgombea katika uchaguzi uliopita wa urais, kwa sasa yuko Morocco. Aliondolewa madarakani katika mazingira tatanishi, aliruhusiwa na viongozi wa mapinduzi kuondoka nchini kuelekea Senegal, ambapo alisafiri hadi Kongo-Brazzaville na kisha hadi Morocco.
Mpinzani wake mkuu katika uchaguzi wa rais wa mwezi Novemba mwaka jana, Fernando Dias da Costa, alikimbilia katika ubalozi wa Nigeria huko Bissau, ambao ulimpa hifadhi wakati wa mapinduzi. Mshirika wake, Domingos Simões Pereira, rais wa Chama cha PAIGC, ambaye ugombea wake ulibatilishwa mnamo mwezi Septemba 2025, bado anashikiliwa nchini Guinea-Bissau.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime