Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakihusiki kwa namna yoyote na uamuzi wa Mahakama Kuu wa kuzuia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kufanya shughuli zake za kisiasa.
Ufafanuzi huo umetolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa CCM Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenan Kihongosi, kufuatia kauli iliyotolewa na Mzee Joseph Butiku Januari 19 mwaka huu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo alihoji uhalali wa CCM kuendelea na shughuli zake wakati CHADEMA kikiwa kimewekewa zuio hivyo chama hicho kimeeleza kuwa zuio hilo limetokana na mgogoro wa ndani wa chama hicho na uamuzi wa mahakama
Kihongosi amesema kuwa zuio la CHADEMA limetokana na uamuzi wa Mahakama Kuu katika shauri la maombi madogo namba 8960 la mwaka 2025, lililofunguliwa na wanachama watatu wa chama hicho ambao ni Said Mohammed, Ahmed Khamis na Maulidah Komu.
Aidha amesema kuwa wanachama hao waliwasilisha maombi mahakamani dhidi ya Wadhamini na Katibu Mkuu wa Chadema wakiomba chama hicho kizuiwe kufanya shughuli zozote za kisiasa pamoja na kutumia mali zake hadi shauri la msingi litakaposikilizwa na kuhitimishwa.
Hata hivyo kwa mujibu wa CCM shauri la msingi ni namba 8323 la mwaka 2025 na Mahakama Kuu baada ya kusikiliza maombi madogo ilitoa uamuzi wa kuzuia CHADEMA kufanya shughuli zote za kisiasa hadi shauri hilo litakapomalizika.
Kutokana na uamuzi huo, CCM imesema siyo chama hicho wala Serikali iliyochukua hatua ya kukizuia CHADEMA, bali ni mchakato wa kisheria uliotokana na mgogoro wa ndani ya chama hicho.
CCM imewataka Watanzania kupuuza taarifa na kauli ilizozieleza kuwa ni za upotoshaji, pamoja na kujiepusha na kauli za chuki zinazoweza kuhatarisha amani na utulivu wa taifa.