Mashambulizi Ukraine na Urusi Yaua Raia na Maafisa

UKRAINE na Urusi zimeripoti vifo na majeruhi kufuatia mashambulizi ya pande zote hali inayoonyesha kuendelea kwa mapigano makali kati ya mataifa hayo mawili.

Kwa upande wa Ukraine raia watatu wameuawa baada ya mashambulizi ya Urusi katika mji wa kusini mashariki wa Zaporizhzhia.

Ambapo Gavana wa mkoa huo Ivan Fedorov amesema mashambulizi hayo pia yamesababisha kukatika kwa umeme katika maeneo kadhaa hali iliyowaacha wakazi bila huduma muhimu.

Fedorov ameongeza kuwa vikosi vya Urusi vimeendelea kulenga miundombinu ya kiraia jambo linalozidisha mateso kwa wananchi wa kawaida.

Nchini Urusi Gavana wa mkoa wa Belgorod ameripoti kifo cha afisa mmoja wa usalama kufuatia mashambulizi yanayodaiwa kutoka Ukraine.

Aidha vifo vingine viwili vimeripotiwa katika mkoa wa Bryansk baada ya mashambulizi ya makombora.

Wakati huohuo watu wanane wamejeruhiwa baada ya kutokea mlipuko katika mji wa Adygea mashariki mwa Bahari Nyeusi huku mamlaka zikianza uchunguzi wa chanzo cha tukio hilo.

Kwa kawaida ni nadra kwa Ukraine kufanya mashambulizi ndani ya ardhi ya Urusi kwani imekuwa ikikabiliana na uvamizi wa Urusi kwa takribani miaka minne sasa na mara nyingi hukabiliwa na changamoto za kijeshi na vifaa.

Hata hivyo mapigano haya yanaendelea kuongeza hofu ya kupanuka kwa vita na kuathiri zaidi usalama wa raia wa nchi zote mbili.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii