MAELFU ya raia wa asili ya Kikurdi wamejitokeza katika maandamano kwenye miji mbalimbali ya Ujerumani wakionyesha mshikamano na wenzao kufuatia mapigano kati ya vikosi vya Wakurdi na wanajeshi wa serikali ya Syria.
Kwa mujibu wa polisi takribani waandamanaji 4,000 waliingia mitaani katika mji wa magharibi wa Dortmund idadi iliyozidi kwa mbali watu 400 pekee waliokuwa wamejisajili kushiriki maandamano hayo.
Maandamano kama hayo yalifanyika pia katika miji ya Frankfurt, Stuttgart Hanover na Bremen yakivuta maelfu ya washiriki.
Katika mji wa kibiashara wa Frankfurt polisi wamesema watu wapatao 5,000 walijitokeza licha ya waandamanaji waliokuwa wamejiandikisha kuwa ni 200 tu.
Mamia ya askari wa polisi walitumwa kulinda usalama wa maandamano hayo ambayo yalifanyika chini ya kaulimbiu ya “Mshikamano na Rojava”, neno linalotumiwa kuelezea maeneo ya Wakurdi yanayojitawala kaskazini na mashariki mwa Syria.
Hatua hiyo inakuja wakati ambapo makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya vikosi vya Wakurdi vinavyoungwa mkono na Marekani na jeshi la Syria yalifikiwa juzi ingawa mamlaka zinasema hali bado ni tete na inaweza kubadilika wakati wowote.
Hata maandamano hayo yanaonyesha wasiwasi wa jumuiya ya Wakurdi barani Ulaya kuhusu mustakabali wa wenzao katika maeneo ya migogoro ya Syria.