Rais mteule wa Chile anayefuata siasa kali za mrengo wa kulia Jose Antonio Kast amewateuwa wanasheria wawili wa dikteta wa zamani wa nchi hiyo, Augusto Pinochet, kuongoza wizara za ulinzi na haki za binaadamu.
Kast, ambaye ataapishwa rasmi tarehe 11 Machi, ni mwanasiasa wa kwanza anayefuata za mrengo huo tangu Pinochet, ambaye utawala wake uliacha makovu mabaya kwa taifa hilo la Amerika Kusini.
Utawala wa kidikteta wa Pinochet kutoka mwaka 1973 hadi 1990 unatuhumiwa kwa kusababisha vifo vya zaidi ya watu 3,200, huku makumi kwa maelfu ya wengine wakipotezwa, kufungwa ama kuteswa kikatili.
Lakini Kast ni shabiki mkubwa wa Pinochet aliyefariki dunia mwaka 2006 akiwa na umri wa miaka 91 bila kushitakiwa.
Mwanasiasa huyo alipata ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi wa mwezi Disemba, akiungwa mkono kutokana na kampeni yake dhidi ya uhalifu na dhidi ya wahamiaji.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime