Kama sehemu ya sheria mpya za uhamiaji zilizoungwa mkono na Rais Donald Trump, Marekani imetangaza kuanzia Jumatano, Januari 21, kusitishwa kwa maombi yote ya visa za kudumu za uhamiaji kutoka nchi 75, ikiwa ni pamoja na mataifa 26 ya Afrika, miongoni mwao Côte d’Ivoire, Cameroon, na Senegal.
Tofauti na visa za watalii, hatua hii inatumika kwa visa zinazoitwa "kukaa kwa muda mrefu", ambazo huruhusu madhumuni kama vile kuungana tena kwa familia au kupata ajira nchini Marekani. Kulingana na Washington, kusitishwa huku kunalenga kuwapa mamlaka muda wa kupitia kwa kina mchakato mzima wa kutoa vibali hivi vya ukaazi.
Katika taarifa ya Januari 7, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani inadai kwamba raia wa nchi zilizolengwa, ambao tayari wanaishi Marekani, wanapokea usaidizi wa kijamii katika "viwango visivyokubalika."
Kwa Donald Trump, wahamiaji lazima sasa wawe "huru kifedha" na sio "mzigo kwa Wamarekani." Kwa hivyo utawala umezindua marekebisho kamili ya Sheria ya Uhamiaji na Uraia, sheria inayosimamia sheria za kupata visa za uhamiaji.
Vigezo vya kustahiki vimetakiwa kubadilika
Kwenye tovuti yake, Wizara ya Mambo ya Nje inabainisha kuwa lengo ni kuhakikisha kwamba "wahamiaji kutoka nchi zilizo katika hatari kubwa hawapati manufaa ya ustawi nchini Marekani." Vigezo vya kustahiki visa hivi vinaweza kubadilika: zaidi ya rasilimali za kifedha, umri na afya ya waombaji sasa vinaweza kuzingatiwa katika tathmini ya maombi.
Hata hivyo, ikiwasilishwa kama ya muda, hatua hii ya usitishwaji inaweza kuwa ya kudumu. Wizara ya Mambo ya Nje imebainisha kuwa kusitishwa kwa maombi kutaendelea kutumika hadi Marekani itakapohakikisha kwamba wahamiaji wapya "hawatapoteza utajiri wa raia wa Marekani." Pia imesema kwamba "itafanya inachokiweza ili kuhakikisha kwamba ukarimu wa watu wa Marekani hautumiwi tena."
Donald Trump alitangaza mwishoni mwa mwezi Novemba 2025 nia yake ya kuimarisha sera ya uhamiaji ya Marekani kwa kiasi kikubwa: "Nitasitisha kabisa uhamiaji kutoka nchi zote za Dunia ya Tatu ili kuruhusu mfumo wa Marekani kupona kikamilifu," aliandika katika ujumbe uliochapishwa kwenye jukwaa laTruth Social, akibainisha kwamba anaweza kufuta "mamilioni" ya vibali vilivyotolewa wakati wa utawala wa rais Joe Biden.
Siku ya Jumatatu Januari 12, 2026, Wizara ya Mambo ya Nje ilitangaza kwamba ilifuta visa zaidi ya 100,000 tangu Trump arudi madarakani. Mnamo mwezi Desemba 2025, Wizara ya Usalama wa Nchi pia ilifichua kwamba utawala uliwafukuza zaidi ya watu 605,000, na kwamba wengine milioni 2.5 waliondoka kwa hiari yao wenyewe.
Orodha ya nchi za Kiafrika zinazolengwa na hatua hii mpya:
Algeria, Cameroon, Cape Verde, Côte d’Ivoire, DRC, Misri, Eritrea, Ethiopia, Gambia, Ghana, Guinea, Liberia, Libya, Morocco, Nigeria, Jamhuri ya Kongo, Rwanda, Senegal, Sierra Leone, Somalia, Sudan Kusini, Sudan, Tanzania, Togo, Tunisia, na Uganda.