Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa serikali yake inachunguza uwezekano wa kufikia makubaliano kuhusu Greenland kufuatia mazungumzo aliyofanya na viongozi wa Jumuiya ya Kujihami ya Atlantiki ya Kaskazini (NATO).
Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii Trump alisema kuwa alifanya mkutano wenye mafanikio makubwa na uongozi wa NATO uliosababisha kuwepo kwa kile alichokiita mfumo wa makubaliano yanayoweza kufikiwa kuhusu Greenland pamoja na eneo pana la Arctic, ingawa hakutoa maelezo ya kina kuhusu maudhui ya mfumo huo.
Katika hatua hiyo, Trump pia aliondoa mipango ya awali ya kuweka ushuru kwa baadhi ya washirika wa Ulaya, waliokuwa wamepinga wazi pendekezo lake la Marekani kumiliki kisiwa cha Greenland.
Kwa upande wake NATO ilithibitisha kufanyika kwa mkutano huo na kuuelezea kuwa “wenye tija kubwa,” ikieleza kuwa majadiliano kuhusu mfumo unaotajwa na Trump yatalenga zaidi kuimarisha usalama wa eneo la Arctic, eneo linalozidi kuwa na umuhimu wa kimkakati kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na ushindani wa kijiografia.
Hapo awali akizungumza katika Jukwaa la Uchumi Duniani (World Economic Forum) lililofanyika Davos, Uswisi, Trump alisisitiza kuwa hatatumia nguvu za kijeshi kufanikisha azma hiyo, bali anataka mazungumzo ya kidiplomasia ili kufikia makubaliano yanayoridhisha pande zote.
Kauli hiyo imeendelea kuzua mjadala mpana kimataifa hasa kuhusu uhuru wa Greenland, msimamo wa Denmark kama dola mama, pamoja na nafasi ya eneo la Arctic katika siasa za kimataifa na maslahi ya kiusalama.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime