Pigo kwa Mudavadi mahakama ikifufua chama chake ANC
MAHAKAMA Kuu imebatilisha kuvunjwa kwa chama cha kisiasa cha Amani National Congress (ANC), kinachohusishwa na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, na kukirejesha rasmi katika ulingo wa siasa.
Katika hatua ambayo ni pigo la kisheria kwa muungano wake na chama cha United Democratic Alliance (UDA), mahakama ilifuta Notisi ya Gazeti la Serikali iliyotolewa mwaka jana na kumuagiza Msajili wa Vyama vya Kisiasa kurejesha mara moja hadhi kamili ya kisheria ya ANC.
ANC kilivunjwa Januari 2025 na kuunganishwa na UDA cha Rais William Ruto, kikafutwa rasmi Machi 7, 2025 baada ya Mkutano Maalum wa Kitaifa wa Wajumbe (NDC) kukubali uamuzi huo.
Kufuatia muungano huo, Gavana wa Lamu Issa Timamy, aliyekuwa kiongozi wa ANC, aliteuliwa kuwa naibu kiongozi wa UDA, huku Mbunge wa Emuhaya Omboko Milemba, aliyekuwa katibu mkuu wa ANC, akichukua wadhifa wa naibu katibu mkuu wa UDA.
Hatua hiyo ilipigwa vita mahakamani na mwanaharakati wa haki za raia Stephen Mutoro, aliyemshtaki Bw Mudavadi, Msajili wa Vyama vya Kisiasa na maafisa wengine wa chama.
Kesi hiyo ilihusu haki za kisiasa za wanachama na mustakabali wa chama kilichoanzishwa kutetea siasa za mageuzi.
Katika uamuzi wake, mahakama ilitangaza kuwa Mkutano Maalum wa NDC uliofanyika Februari 7, 2025 ulikuwa kinyume cha sheria, ikisema uliendeshwa “kwa kukiuka Katiba” kwa kukosa kuwahusisha wanachama.
Maamuzi yote yaliyofikiwa katika mkutano huo, yakiwemo kuvunjwa kwa chama na kuhamisha mali yake, yalitangazwa kuwa kinyume cha Katiba, haramu, batili na yasiyo na nguvu ya kisheria tangu mwanzo.
Mahakama pia ilifuta Notisi ya Gazeti Na. 3449 ya Machi 7, 2025 iliyorasmisha kuvunjwa kwa ANC.
“ANC bado ni chama cha kisiasa kilichosajiliwa kihalali ambacho uhai wake wa kisheria haujawahi kukomeshwa kwa njia halali,” alisema Jaji Bahati Mwamuye.
Jaji huyo alitoa amri inayomlazimisha Msajili wa Vyama vya kisiasa, kufuta rekodi zote za kuvunjwa kwa chama na kutoa taarifa kwa taasisi za serikali na umma.
Aidha, alitoa amri ya kudumu ya kuzuia wahusika kuingilia mali ya ANC kama ilivyokuwa Februari 6, 2025 bila kufuata sheria, na akaagiza mali yoyote iliyohamishiwa UDA au taasisi nyingine irejeshwe mara moja.
Mzozo huo ulitokana na migawanyiko ya ndani ya ANC baada ya Bw Mudavadi kujiunga na kambi ya Rais Ruto na kuunga mkono muungano na UDA.
Wakosoaji ndani ya chama walidai mchakato huo uliwatenga wanachama wa mashinani na kupuuza taratibu za kikatiba.
Uamuzi huo haujarejesha tu hadhi ya ANC bali pia unatatiza uundaji wa miungano ya kisiasa kuelekea uchaguzi wa 2027, huku ukisisitiza umuhimu wa demokrasia ya ndani na ushiriki wa wanachama katika maamuzi makubwa ya vyama vya kisiasa.
Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii