Ikiwa ni Wiki moja baada ya uchaguzi nchini Uganda ambapo kesi ya mwanasheria na mwanaharakati wa haki za binadamu Sarah Bireete bado inaendelea huku mahakama ikiahirisha uamuzi wake kuhusu dhamana hadi Januari 28.
Mahakama ya Buganda Road ilisema inahitaji muda zaidi kuchunguza hoja zilizowasilishwa na upande wa mashtaka na ule wa utetezi. Sarah Bireete, aliyekamatwa Desemba 30 mjini Kampala alifikishwa mahakamani siku ya Januari 21 mwaka huu akituhumiwa kwa “kufichua data ya wapiga kura bila idhini ya Tume ya Uchaguzi”—tuhuma anazikana vikali.
Awali hoja za mashtaka na utetezi zilieleza Mahakamani hapo kuwa pande zote mbili zilikabiliana hoja kwa hoja. Upande wa utetezi uliwasilisha sababu za kimatibabu, ukidai kuwa Sarah Bireete anaugua shinikizo la damu na anahitaji matibabu maalum nje ya gereza.
Hata hivyo, upande wa mashtaka ulipinga hoja hiyo, ukisema kuwa “hakuna ushahidi kwamba Mamlaka ya Magereza haiwezi kumpatia matibabu yanayohitajika.” Mashtaka pia yalieleza wasiwasi kuhusu hatari ya kuingilia mashahidi na kuhoji uwezo wa kifedha wa wadhamini waliopendekezwa.
Wafuasi wa mwanaharakati huyo wameendelea kulaani kuendelea kwake kuzuiliwa, wakidai ni hatua ya kisiasa inayolenga kuwanyamazisha wakosoaji wa serikali baada ya uchaguzi.
Akizungumza kuhusu suala hilo, Agather Atuhaire anahoji msingi wa mashtaka hayo:
“Kwa kweli, huu ni uhalifu gani? Taarifa hizi zilichukuliwa kutoka kwenye tovuti ya Tume ya Uchaguzi na kushirikiwa na umma. Zilitakiwa kuwa wazi kwa kila mtu,” alisema.
Anaongeza kuwa kucheleweshwa kwa kuachiliwa kwa Sarah Bireete kunahusiana moja kwa moja na mazingira ya kisiasa baada ya uchaguzi.
“Ukandamizaji baada ya uchaguzi, kwa maoni yangu, ni mbaya zaidi kuliko hapo awali. Inaonekana kuna nia ya kuendelea kuwazuia wale wote wanaokosoa kinachoendelea hivi sasa,” aliongeza.
Aidha kupitia hatua hiyo ambayo kamatakamata inaongezeka baada ya uchaguzi Agather Atuhaire anaelezea hali ya sasa nchini Uganda kama kipindi cha ukandamizaji mkubwa, akidai kuwa kamatakama imeongezeka, hasa miongoni mwa wafuasi wa upinzani. Vurugu pia zimeripotiwa katika vitongoji kadhaa vya miji mikubwa.
Kwa mujibu wake, Sarah Bireete alizuiliwa kwa siku kadhaa bila mashtaka kabla ya kufikishwa mahakamani, na mahakama tayari iliwahi kuipa ofisi ya mwendesha mashtaka wiki kadhaa kujibu ombi la dhamana.
Hivyo uamuzi wa dhamana ya Sarah Bireete sasa unasubiriwa kwa hamu, huku kesi yake ikionekana kuwa kielelezo cha mvutano wa kisiasa na haki za binadamu nchini Uganda baada ya uchaguzi.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime