Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita amefanya ziara ya dharura katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala Wilaya ya Kahama kukagua na kujionea athari za mvua kubwa zilizoonyesha usiku wa kuamkia Desemba 12, na kuleta madhara katika maeneo kadhaa ya makazi na miundombinu ya huduma kwa wananchi.
Mhita akiwa kwenye ziara hiyo ameonyesha kuguswa na hali ya wananchi waliopatwa na madhara mbalimbali, akitoa maelekezo ya haraka kwa viongozi wa halmashauri kuhakikisha kuwa wananchi wote walioumia au kupata majeraha kutokana na athari hizo, wanapatiwa matibabu bure katika vituo vya afya vilivyo karibu.
Akitembelea Kituo cha Afya Mwanase kilichoathiriwa na mvua, Mhita ameagiza kituo hicho kutoendelea kutoa huduma za uzazi katika eneo lililoathirika, kutokana na kuwa hatarishi kwa usalama wa akina mama wajawazito, ameagiza eneo hilo kufanyiwa ukarabati wa haraka na kuimarishwa kabla ya kuanza kutumika tena.
Aidha, Mhita amemuelekeza Mhandisi wa Halmashauri ya Msalala kupitia upya majengo yote ya umma, hususan yale yanayojengwa kwa nguvu za wananchi, kabla hayajaanza kutumika, ili kuhakikisha yanazingatia viwango na usalama unaohitajika.
Mkuu wa Mkoa pia amesisitiza msimamo wa Serikali ya Mkoa wa Shinyanga wa kuwalinda wananchi wake dhidi ya athari za majanga ya asili na kuhakikisha utoaji wa huduma za msingi haukwami hata katika mazingira ya dharura.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala, Abdulkadir Mfilinge, amesema kuwa huduma za afya kwa sasa zimehamishiwa kwenye zahanati ya karibu, huku juhudi za awali za tathmini na maandalizi ya ukarabati zikianza mara moja kwa kushirikiana na wataalamu wa sekta husika.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime