Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki jijini Dar es Salaam, Kardinali Polycarp Pengo amefariki dunia usiku wa Februari 19, 2026, alipokuwa akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam.
Taarifa ya kifo chake imetolewa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Yude Ruwai’chi, aliyeeleza kuwa Kanisa Katoliki nchini limepoteza kiongozi wake mashuhuri aliyetoa mchango mkubwa katika huduma ya kiroho na maendeleo ya jamii kwa miongo kadhaa.
Kardinali Pengo alizaliwa mwaka 1944 katika Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro.
Alipata daraja takatifu ya upadre mwaka 1971 na baadaye kuwekwa wakfu kuwa Askofu mwaka 1983.
Mwaka 1992 aliteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, nafasi aliyohudumu kwa zaidi ya miaka 27 hadi alipostaafu mwaka 2019.
Katika kipindi cha utumishi wake, alijulikana kwa msimamo wake thabiti juu ya maadili ya jamii, amani na mshikamano wa kitaifa.
Mwaka 1998 aliteuliwa kuwa Kardinali na Papa Yohane Paulo II, hatua iliyomuweka miongoni mwa viongozi wakuu wa Kanisa Katoliki duniani.
Mbali na majukumu ya kichungaji, Kardinali Pengo alishiriki katika mijadala mbalimbali ya kijamii na kitaifa, akihimiza maadili, uwajibikaji na mshikamano miongoni mwa Watanzania bila kujali tofauti za kidini au kisiasa.
Aidha kanisa Katoliki linatarajiwa kutoa ratiba ya mazishi na taratibu nyingine rasmi baadaye.
Hata hivyo waumini na wananchi kwa ujumla wameendelea kutuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha kiongozi huyo wa kiroho aliyelitumikia taifa kwa uadilifu na kujituma kwa muda mrefu.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime