Polisi wa Afrika Kusini wamekamata mtoto wa kiongozi wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe

Mtoto mdogo wa rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe amekamatwa baada ya mtunza bustani kupigwa risasi nyumbani kwake Afrika Kusini, polisi na wakili wa familia wamesema.

Wakili Ashley Mugiya ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba Bellarmine Chatunga Mugabe alikuwa mmoja wa wanaume wawili waliokamatwa na kuhojiwa siku ya Alhamisi.

Polisi ya Afrika Kusini imesema kwamba wanaume wote wawili walikamatwa baadaye na watakabiliwa na mashtaka ya kujaribu kuua.

Mamlaka ilithibitisha kwamba mfanyakazi katika nyumba hiyo alikuwa na jeraha moja la risasi na alikuwa katika hali mbaya, ingawa haikuwa wazi ni risasi ngapi kwa jumla zilipigwa.

"Lengo la shambulio hilo halijulikani kwa sasa, na uchunguzi wa polisi unaendelea," Kanali Dimakatso Nevhuhulwi amesema.

Polisi hawakuwataja wanaume hao wawili waliokamatwa, ingawa polisi wa Afrika Kusini kwa kawaida hukataa kuwataja washukiwa hadi watakapofika mahakamani na kushtakiwa rasmi.

Shirika la utangazaji la Afrika Kusini, SABC, limesema tukio hilo la ufyatuaji risasi lilitokea nyumbani kwa mtoto huyo wa Robert Mugabe, katika kitongoji cha kifahari cha Johannesburg.

Nevhuhulwi amesema kwamba washukiwa wote wawili hawakuwa na ushirikiano polisi walipofika eneo la tukio kwa mara ya kwanza.

"Hawajatuambia bunduki hiyo iko wapi," Nevhuhulwi amesema. "Hatuwezi kusema ni nani aliyepiga risasi."

Mugiya, wakili anayeishi Zimbabwe, amesema mawakili nchini Afrika Kusini wangemwakilisha Mugabe katika kesi hiyo.

Kiongozi wa zamani wa Zimbabwe

Bellarmine Chatunga Mugabe ndiye mtoto wa mwisho wa kiongozi wa zamani wa Zimbabwe, aliyefariki Singapore mwaka wa 2019, na mkewe wa pili, Grace Mugabe. Kiongozi huyo wa Zimbabwe aliondolewa madarakani mwaka wa 2017 baada ya miaka 37 madarakani.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii