Mtoto wa Mugabe Akamatwa kwa Jaribio la Mauaji

Polisi nchini Afrika Kusini wamemkamata Bellarmine Mugabe, mtoto wa mwisho wa aliyekuwa Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, kwa tuhuma za kujaribu kuua kufuatia tukio la ufyatuaji risasi lililoripotiwa katika kitongoji cha kifahari cha Hyde Park, jijini Johannesburg.

Kwa mujibu wa polisi Bellarmine mwenye umri wa miaka 28 alikamatwa baada ya mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka 23, anayedaiwa kuwa mtunza bustani, kupigwa risasi na kujeruhiwa katika tukio hilo.

Ambapo maafisa wa polisi walifanya upekuzi nyumba aliyokuwa akiishi Mugabe walipata risasi na hawakufanikiwa kukuta bunduki iliyotumika katika tukio hilo ingawa uchunguzi zaidi unaendelea ili kubaini chanzo na mazingira ya tukio hilo.

Lakini pia Mwanamume mwingine  amekamatwa kuhusiana na tukio hilo, huku msemaji wa polisi, Kanali Dimakatso Nevhuhulwi, akithibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao na kueleza kuwa uchunguzi bado unaendelea.

Aidha itakumbukwa kuwa Bellarmine Mugabe ni mtoto wa mwisho wa Robert Mugabe na mkewe wa pili, Grace Mugabe. Robert Mugabe aliiongoza Zimbabwe kwa kipindi cha miaka 37 kabla ya kuondolewa madarakani mwaka 2017, na alifariki dunia mwaka 2019 akiwa na umri wa miaka 95.

Hata hivyo Polisi wamesema kuwa watatoa taarifa zaidi mara baada ya uchunguzi kukamilika.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii