Marekani Yasema Iko Tayari Kuchukua Hatua Dhidi ya Iran Kuzuia Silaha za Nyuklia

Waziri wa Ulinzi wa Marekani amesema kuwa jeshi la nchi hiyo lipo katika utayari kamili kutekeleza uamuzi wowote utakaochukuliwa na Rais Donald Trump kuhusu Iran, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuizuia Tehran kupata silaha za nyuklia.

Akizungumza katika mkutano wa Baraza la Mawaziri, Rais Trump aliomba tathmini kutoka kwa Waziri wa Ulinzi, Pete Hegsett, kuhusu uwepo na uwekaji wa wanajeshi wa Marekani katika eneo la Ghuba ya Uajemi (Persian Gulf).

Kwa mujibu wa maafisa wa Marekani, Rais Trump bado anaendelea kuchambua chaguzi mbalimbali, ikiwemo hatua za kidiplomasia na kijeshi, ingawa bado hajafikia uamuzi wa mwisho kuhusu uwezekano wa kufanya shambulio la moja kwa moja dhidi ya Iran.

Mvutano kati ya Marekani na Iran umeendelea kuongezeka katika wiki za hivi karibuni, hali inayochangiwa na hatua kali za Serikali ya Iran dhidi ya maandamano yenye vurugu ndani ya nchi hiyo, pamoja na kuendelea kwa mpango wake wa nyuklia.

Hata hivyo Rais Trump ameonya kuwa Marekani haitasita kuchukua hatua iwapo Tehran itaendelea na juhudi za kutengeneza silaha za nyuklia, kauli inayokuja kufuatia mashambulio ya anga yaliyoripotiwa kufanywa na Israel na Marekani yakilenga maeneo muhimu yanayohusishwa na mpango wa nyuklia wa Iran.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii