Senegal: Serikali inapanga kukata rufaa dhidi ya vikwazo vya CAF dhidi ya kocha Pape Thiaw

Kufuatia vikwazo vilivyotangazwa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), siku kumi na moja baada ya mchezo wa fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika uliokuwa na ushindani mkubwa nchini Morocco, Senegal inapambana. Dakar inasema inakusudia kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa CAF wa kumsimamisha kocha Pape Thiaw kwa mechi tano na kumtoza faini ya dola 100,000, au takriban faranga za CFA milioni 54.


Hii ni mojawapo ya chaguzi zinazopatikana kwa Shirikisho la Soka la Senegal wa kukata rufaa dhidi ya vikwazo vilivyowekwa na CAF dhidi ya Senegal na haswa zaidi kwa kocha Pape Thiaw, kwa tume au Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo jamba ambalo  ndiyo chaguo lililoidhinishwa na serikali, kama ilivyotangazwa kwa vyombo vya habari na Waziri wa Vijana na Michezo wa Senegal, Khady Diene Gaye.

"Tutafanya kila liwezekanalo kupunguza adhabu hii. Ninaamini si kwa maslahi ya timu yetu kumuona kocha wetu akiketi kwenye benchi (akishangilia kama mashambiki wa kawaida) kwa mechi tano za CAF, pamoja na faini. Kocha alijiendesha kama Msenegali wa kweli. Kocha wetu alijifanya kama mzalendo wa kweli. Tutafanya juhudi zozote kumtetea."

Kampeni ya kuchangisha fedha imezinduliwa ili kumuunga mkono Thiaw ambaye anatoa wito wa michango kuelekezwa badala yake kwa "sababu za dharura zaidi." Pape Bouna Thiaw anasalia kuwa shujaa machoni pa raia wa Senegal, baada ya kuwaongoza Simba kwenye taji lao la pili la bara katika historia yao. Uthibitisho wa hili ni uchangishaji fedha mtandaoni uliozinduliwa na mashabiki ili kumsaidia kocha kulipa faini ya faranga za CFA milioni 54 kama faini, iliyotozwa na CAF. Ndani ya saa chache, faranga milioni 2 za CFA zilikuwa tayari zimekusanywa, kabla ya Pape Thiaw mwenyewe, kupitia akaunti yake ya Instagram, kuwaomba raia wa Senegal kuelekeza pesa hizo kwa sababu muhimu zaidi:

"Mshikamano wenu tangu kutangazwa kwa vikwazo unanigusa sana. (...) Hata hivyo, ninawaomba kwa unyenyekevu msipange michango ya fedha kwa jina langu. Ingawa ninaelewa na kuthamini ukarimu huu mkubwa, ninawasihi mrejeshe fedha hizi kwa sababu za dharura zaidi, kwa manufaa ya wale wanaozihitaji kweli."

Mbali na Pape Thiaw, wachezaji Illiman Ndiaye na Ismaïla Sarr walipokea adhabu za mechi mbili. Illiman Ndiaye alipewa adhabu kwa kumwita mwamuzi wa mchezo wa fainali "fisadi," na Ismaïla Sarr kwa "tabia isiyo ya kawaida kwa mwamuzi." Shirikisho la Soka la Senegal litalazimika kulipa faini ya dola 15,000 kwa "utovu wa nidhamu wa timu ya taifa," pamoja na dola 300,000 kwa ukosoaji uliotolewa na rais wake, Abdoulaye Fall, dhidi ya CAF (Shirikisho la Soka la Afrika), na dola 300,000 nyingine kutokana na "tabia isiyofaa ya mashabiki wake" wakati wa mchezo wa fainali; makabiliano makubwa, ikiwa ni pamoja na jaribio la uvamizi wa uwanja, yalizuka wakati wachezaji wa Senegal walipoamua kuondoka uwanjani.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii