Jeshi la Polisi limetoa taarifa rasmi kuelekea mchezo wa kimataifa wa Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Young Africans SC na Al Ahly ya Misri unaotarajiwa kuchezwa katika Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Katika taarifa hiyo Jeshi la Polisi limesema limejipanga kikamilifu kuhakikisha usalama wa wachezaji, viongozi wa timu, waamuzi pamoja na mashabiki wote watakaohudhuria katika mchezo huo kuanzia kabla, wakati na baada ya mechi.
Aidha polisi imewataka mashabiki wa soka kuzingatia sheria, taratibu na maelekezo yatakayotolewa na vyombo vya ulinzi na usalama, ikiwemo kufika uwanjani mapema kwa ajili ya ukaguzi, kuepuka kubeba vitu hatarishi, na kuacha tabia zozote zinazoweza kuhatarisha amani na usalama.
Hata hivyo Jeshi la Polisi limesisitiza kuwa halitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya mtu yeyote atakayekiuka sheria au kujaribu kuvuruga amani wakati wa mchezo huo mkubwa unaofuatiliwa na mashabiki wengi ndani na nje ya nchi.
