Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limechukua hatua kali dhidi ya timu za Senegal na Morocco kufuatia vurugu zilizojitokeza katika mchezo wa fainali ya AFCON 2025 uliofanyika nchini Morocco.
Kwa upande wa Senegal, kocha Pape Thiaw amefungiwa mechi tano za mashindano rasmi na kutozwa faini ya dola 100,000 za Marekani. Wachezaji Malick Ndiaye na Ismaila Sarr wamefungiwa mechi mbili kila mmoja.
Vilevile, Shirikisho la Soka la Senegal limepigwa faini ya dola 300,000 kwa vurugu za mashabiki, dola nyingine 300,000 kwa vurugu za wachezaji na benchi la ufundi, pamoja na faini ya dola 15,000 kwa wachezaji waliopata kadi nyingi za onyo.
Kwa jumla Senegal wanapaswa kulipa dola 615,000.
Kwa upande wa Morocco, nyota Achraf Hakimi amefungiwa mechi mbili, huku adhabu ya mechi moja ikitekelezwa mara moja na nyingine kuwa chini ya uangalizi kwa mwaka mmoja.
Mchezaji Ismael Saibari amefungiwa mechi tatu na kutozwa faini ya dola 100,000.
Shirikisho la Soka la Morocco pia limepigwa faini ya dola 315,000 kutokana na vurugu za mashabiki, wachezaji na matumizi ya tochi uwanjani.
CAF imesisitiza kuwa adhabu hizo ni ujumbe mzito kwamba vurugu na tabia zisizo za kimichezo hazina nafasi katika soka la Afrika, na kwamba nidhamu na heshima kwa wachezaji, benchi la ufundi na mashabiki ni msingi wa mashindano ya kimataifa.