RC Iringa asisitiza wananchi kuwalinda wakandarasi na vifaa vya ujenzi

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Kheri James, amewataka wananchi wa Mkoa huo kutoa ushirikiano kwa Wakandarasi wa miradi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), ikiwemo kulinda miundombinu na vifaa vya ujenzi ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati na iweze kuleta tija na kuchochea maendeleo nchini.

RC James amebainisha hayo leo Januari 29, 2026 wakati Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ikimtambulisha rasmi mkandarasi; kampuni ya M/s Silo Power itakayotekeleza Mradi wa Kusambaza Umeme kwenye vitongoji 214 vya mkoa wa Iringa ambapo mradi huo unatarajiwa kutekelezwa katika kipindi cha miaka mitatu, kuanzia sasa.

Vile vile, RC James amesema mkoa wa Iringa unamahitaji makubwa ya umeme kutokana na kuongezeka kwa viwanda vidogo na vya kati na kwamba hiyo ni fursa kwa Wananchi kukuza uchumi na maendeleo kwa ujumla.

“Namshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wanna Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa kipaumbele kwenye Sekta ya Nishati hususan katika Sekta ya nishati; nikitoa mfano kwenye usambazaji wa umeme kwenye vijiji, Iringa vijiji vyote 360 vilishaunganishwa na huduma ya umeme na sasa tunapokea Mradi wenye thamani ya shilingi bilioni 32.3 na wananchi zaidi ya 7,500 watanufaika”. Amesema RC James.

Katika hatua nyingine, RC James amemtaka na kumsisitiza mkandarasi wa mradi huo kuhakikisha anatoa kipaumbele cha ajira kwa wazawa wanaozunguka eneo la mradi ili wananchi hao pia waweze kunufaika na miradi hiyo na kuchochea shughuli za kijamii na kiuchumi mkoani Iringa.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa REA, Bw. Frank Mugogo amesema kuwa vitongoji 1,458 tayari vimefikiwa na huduma ya umeme mkoani Iringa na ambavyo havina umeme ni vitongoji 382. Ameongeza kuwa REA itaendelea kusimamia miradi yote inayotekelezwa nchini kwa weledi ili iweze kukamilika kwa wakati na kuwaomba vingozi wa Serikali ya kijiji na wananchi walioshiriki katika kikao hicho kutoa ushirikiano kwa wakandarasi ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati.

Kwa upande wake, Mha. Mmbalo Msuya kutoka kampuni ya M/s Silo Power amesema kampuni yao, imejipanga ili kukamilisha Mradi wa kusambaza umeme kwenye vitongoji 214 vya mkoa wa Iringa kwa wakati na kuongeza kuwa maelekezo ya RC James ya kutoa ajira kwa wazawa yatapewa kipaumbele ili wananchi wanaozunguka miradi hiyo waweze kunufaika.

Mradi wa bilioni 32.3 kusambaza umeme kwenye vitongoji 214 vya mkoa wa Iringa

Mkandarasi M/s Silo Power atakiwa kumaliza kazi kwa wakati

Wateja 7,500 wataunganishiwa huduma ya umeme

Asema umeme ni maendeleo, uchumi, huduma na biashara

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii