Wakala wa Taifa wa Udhibiti wa Afya wa Brazil imeruhusu rasmi kilimo cha mmea wa Cannabis sativa nchini Brazil kwa matumizi ya tiba na utafiti wa kisayansi.
Uamuzi huo umetokana na maelekezo ya Mahakama ya Juu ya Haki (STJ), ambayo mwezi Novemba 2024 ilithibitisha uhalali wa uzalishaji wa bangi kwa madhumuni ya tiba na/au dawa pekee, kama sehemu ya kulinda haki ya afya.
Kwa matumizi ya tiba, wakurugenzi wa Anvisa wameidhinisha kwa kauli moja kilimo cha katani ya viwandani (industrial hemp), aina maalumu ya Cannabis sativa yenye kiwango cha tetrahydrokannabinoli (THC) kisichozidi asilimia 0.3.
THC ndiyo kiungo kikuu cha mmea kinachosababisha athari za kisaikolojia.
Aina hii ya bangi haisababishi kulevya, lakini ina kiwango kikubwa cha cannabidiol (CBD), ambayo inathaminiwa kwa uwezo wake wa tiba katika kusaidia wagonjwa wenye wasiwasi (anxiety), maumivu sugu, kifafa, matatizo ya usingizi, pamoja na magonjwa mengine ya mfumo wa neva.
Kwa mujibu wa kanuni zilizowekwa, uzalishaji utakuwa na mipaka kulingana na mahitaji ya dawa, na kampuni zitawajibika kutoa taarifa na sababu za kiasi kinachozalishwa, ikiwemo ukubwa wa ardhi (hekta) itakayotumika kwa kilimo.
Kilimo hicho hakijaruhusiwa kwa umma kwa ujumla, bali kinaruhusiwa kwa kampuni na mashirika maalumu pekee, na hatua hii haijumuishi matumizi ya burudani ya bangi.