Ndege ya abiria yaanguka Colombia watu wote 15 wafariki dunia

Ndege ya abiria imeanguka kaskazini mwa Colombia, na kuwaua watu wote 15 waliokuwemo, shirika la ndege la serikali la nchi hiyo, Satena, limethibitisha.

Katika taarifa, shirika hilo lilisema ndege yake aina ya Beechcraft 1900”, ilipata ajali mbaya,” lakini halikutoa maelezo zaidi. Mabaki ya ndege hiyo sasa yamepatikana katika eneo la milima.

Orodha rasmi ya abiria inajumuisha mbunge Diógenes Quintero Amaya na Carlos Salcedo, mgombea katika uchaguzi ujao wa bunge.

Awali, Satena ilisema mawasiliano na ndege hiyo yalikatika dakika 11 kabla ya muda uliopangwa wa kutua katika mji wa Ocaña, karibu na mpaka wa Venezuela, saa 12:05 kwa saa za eneo (17:05 GMT) siku ya Jumatano.

Kwa mujibu wa shirika la ndege, Safari ya NSE 8849 iliondoka katika mji wa Cúcuta, takribani kilomita 100 (maili 62) kaskazini-mashariki mwa Ocaña, ikiwa imebeba abiria 13 na wahudumu wawili wa ndege.

Operesheni ya utafutaji miili imeanzishwa katika eneo la milima, na namba ya simu ya dharura imewekwa kwa ajili ya ndugu wa waliokuwemo ndani ya ndege.

Akizungumza na chombo cha habari cha ndani, Semana, gavana wa Norte de Santander, William Villamizar, alisema miili saba imepatikana.

Taarifa ya kuthibitisha kifo cha Quintero imeshirikiwa kupitia ukurasa wake wa Facebook, ikimuelezea kama “mtu ambaye katika maisha yake yote aliwahudumia wale waliokuwa na uhitaji mkubwa zaidi.”

Quintero alikuwa akishikilia kiti kimoja kati ya viti 16 katika bunge la Colombia vilivyotengwa kuwakilisha waathirika wa mgogoro kati ya jeshi la waasi wa Kimaaandiko ya Marx, Vikosi vya Mapinduzi vya Silaha vya Colombia (FARC), na serikali ya Colombia.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii