Imefahamika kwamba wanamgambo wa RSF nchini Sudan walifaya mauaji ya watu wengi katika jimbo la Darfur na kisha kujaribu kuficha ushahidi kwa kuwazika kwenye makaburi ya pamoja.
Naibu Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, Nazhat Shameem Khan, alilieleza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba ofisi yake "inaamini kuwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu ulitendeka" wakati RSF ilipotwaa udhibiti wa mji mkuu wa Darfur El-Fasher mnamo mwezi Oktoba.
Hivyo kupitia hotuba yake ya Januari 19 mwaka huu iliyofanyika kwa njia ya video Khan alisema kuwa wana ushahidi wa sauti na picha za video za satalaiti ili kuthibitisha tuhuma zao.
Hivyo tangu Aprili 2023 vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya jeshi rasmi la serikali na waasi hao wa RSF vimeshauwa maelfu ya raia na kuwasababisha wengine milioni 11 kuwa wakimbizi, katika kile Umoja wa Mataifa unachosema ni mzozo mkubwa zaidi wa wakimbizi na njaa duniani kwa sasa.
Hata hivyo kumekuwa na ripoti za mauaji ya halaiki ubakaji utekaji na wizi tangu RSF kuutwaa mji wa El-Fasher iliyokuwa ngome ya mwisho ya jeshi la serikali jimboni Darfur na kwamba pande zote mbili zinashutumiwa kutenda ukatili kwenye vita hivyo.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime