Iran imetishia kushambulia miundombinu ya mafuta katika nchi jirani kufuatia mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Israel dhidi ya maeneo ya nishati ndani na karibu na mji mkuu wa Tehran.
Mashambulizi hayo yaliripotiwa kulenga angalau maeneo matano ya nishati, hali iliyosababisha moshi mzito mweusi kutanda angani na kuongeza hofu kuwa mzozo huo unaweza kuathiri vibaya uchumi wa dunia kupitia kupanda kwa bei ya mafuta.
Msemaji wa Islamic Revolutionary Guard Corps (IRGC) alisema iwapo mashambulizi yataendelea, bei ya mafuta duniani inaweza kupanda hadi zaidi ya dola 200 kwa pipa.
Wakati huo huo, United States ilijaribu kutuliza masoko ya kimataifa kwa kueleza kuwa haitalenga miundombinu ya nishati ya Iran.
Kwa mujibu wa kampuni ya usambazaji wa mafuta ya Iran, wafanyakazi wanne walifariki dunia baada ya mashambulizi hayo yaliyosababisha maghala manne ya kuhifadhi mafuta kushambuliwa na moto mkubwa kutokea, huku moshi mzito ukionekana juu ya jiji la Tehran.
Milipuko pia ilisikika katika mji wa Karaj ulio karibu na Tehran, ambapo moshi mkubwa uliripotiwa kufunika baadhi ya maeneo.
Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran amesema nchi hiyo italipiza kisasi endapo mashambulizi dhidi ya miundombinu yake ya nishati yataendelea, huku akizishutumu Israel na Marekani kwa kulenga raia pamoja na vituo vya mafuta.