Iran Yawakamata Viongozi Wanne Wanaodaiwa Kujihusisha Na Vurugu

Iran imewakamata viongozi wanne wa kisiasa wenye mwelekeo wa mageuzi, akiwemo katibu mkuu wa chama cha reformist na aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, katika kile mamlaka za nchi hiyo zimeeleza kuwa ni hatua ya kuzuia jaribio la kuvuruga utaratibu wa kisiasa na kijamii wa taifa.

Kwa mujibu wa maelezo ya vyombo vya usalama na mahakama vimeeleza kuwa  watu hao walikamatwa baada ya uchunguzi uliofanyika kwa miezi kadhaa, uliolenga kufuatilia mienendo ya wanasiasa na wanaharakati waliodaiwa kupanga na kuratibu shughuli za kisiasa nje ya mfumo rasmi wa serikali. Inadaiwa walihusika katika mikutano, mawasiliano na kupanga mikakati ya kuchochea maandamano na kueneza ujumbe uliolenga kuhamasisha raia kupinga uongozi wa nchi.

Mamlaka zinasema waliokamatwa walitumia uzoefu wao wa kisiasa, nafasi walizowahi kushika serikalini, pamoja na ushawishi wao katika vyama na mitandao ya kijamii, kuathiri maoni ya umma na kuhalalisha harakati zilizotafsiriwa kama tishio kwa usalama wa taifa.

Baadhi yao wanadaiwa kuwa na mawasiliano na makundi ya upinzani yaliyo nje ya Iran, madai ambayo serikali imekuwa ikiyatumia mara kwa mara kuhalalisha hatua kali dhidi ya wapinzani wa ndani.

Hata hivyo kukamatwa huku kunajiri wakati Iran ikiendelea kukabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi, ikiwemo kupanda kwa bei za bidhaa muhimu, ukosefu wa ajira, na athari za vikwazo vya kimataifa.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii