Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, ameagiza miradi yote inayotekelezwa katika sekta ya elimu ya msingi ikamilike ifikapo Machi 28, 2026.
Agizo hilo amelitoa leo, Februari 09, 2026, alipokuwa akikagua ujenzi wa Shule Mpya ya Msingi Bukanda iliyopo Kata ya Bukanda, Wilaya ya Ukerewe.
Mhe. Mtanda amesema Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa zaidi ya shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu Wilaya ya Ukerewe, ambapo miradi hiyo inaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
“Serikali imewekeza fedha nyingi katika sekta ya elimu ya msingi, hivyo ni muhimu miradi ikamilike kwa wakati ili wananchi wanufaike na huduma bora za elimu,” amesema Mtanda.
Ametoa wito kwa halmashauri zote za Mkoa wa Mwanza kuhakikisha miradi hiyo inasimamiwa ipasavyo, akiwataka Wakurugenzi Watendaji, Wakuu wa Idara, Watendaji wa Kata na Vijiji kushirikiana kwa karibu ili kufanikisha utekelezaji wake.
Aidha amesema serikali imetoa shilingi milioni 201 kwa ajili ya miradi ya elimu sekondari Ukerewe, na kusisitiza usimamizi wa karibu ili kuepusha miradi kukwama.
“Hatutaki kuona miradi ikiishia nusu. Tutasimamia kwa karibu na nitaita kikao cha mkoa kutathmini utekelezaji wake. Hakuna kubweteka,” ameongeza.
Katika hatua nyingine, Mtanda amewapongeza wananchi wa Ukerewe kwa kuitikia zoezi la uandikishaji wanafunzi, akibainisha kuwa kwa Darasa la Awali uandikishaji umefikia asilimia 105, Darasa la Kwanza asilimia 94 na Kidato cha Kwanza asilimia 85.
Kwa taarifa zaidi tufuatilie na usikilize jembe Habari Kamili hapo saa moja kamili jioni ambapo msomaji wetu wa hii leo ni @jacobmlay__ tafadhali usipitwe na taarifa zetu Mahiri kabisa.
Vilevile tufuatilie kwenye mitandao ya kijamii @ Jembefmtz
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime