Ukraine imesema mashambulizi yaliyofanywa na Urusi yamewaua watu wanne katika miji mbalimbali ya nchi hiyo. Urusi imetumia makombora na ndege zisizo na rubani kuishambulia Ukraine.
Maafisa wa Ukraine wamesema hivi leo kwamba idadi kubwa ya ndege zisizo na rubani za Urusi na makombora yaliyolenga Ukraine yamewaua watu wasiopungua wanne katika miji kote nchini, akiwemo mvulana wa miaka 10.
Waandishi wa habari wa AFP katika eneo la shambulizi moja katika mji wa kusini wa Odesa, wameshuhudia majengo yaliyobomoka na maafisa wa huduma za zimamoto na dharura wakifanya kazi kumhudumia mmoja wa waathiriwa.
Jeshi la anga la Ukraine limesema Urusi ilikuwa imerusha makombora 11 ya masafa marefu na ndege zisizo na rubani 149 , ikiwemo ndege za kivita chapa Shahed zilizotengenezwa na Iran, kuanzia Jumapili jioni hadi alfajiri kuamkia leo Jumatatu.
Waandishi hao pia wamesema vikosi vya ulinzi wa anga vilizidungua zaidi ya ndege zisizo na rubani mia moja na makombora kadhaa, lakini hawakutoa ufafanuzi.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime