CPJ: Waandishi wa Kipalestina wanateswa magerezani Israel

Kamati ya Kimataifa ya Kuwalinda Waandishi wa Habari - CPJ imesema waandishi habari wa Kipalestina waliofungwa katika magereza ya Israel kuanzia Oktoba 2023 hadi Januari 2026 wamepitia "unyanyasaji wa kimfumo."

Taarifa ya shirika hilo lenye makao yake makuu jijini New York imesema kati ya waandishi 59 waliohojiwa, wote isipokuwa mmoja walisema walifanyiwa kile walichoelezea kuwa ni mateso, unyanyasaji au aina nyingine ya ukiukaji. Mkurugenzi wa CPJ Jodie Ginsberg ameihimiza jumuiya ya kimataifa "kuchukua hatua" kuhusu ripoti hizo za unyanyasaji.

Shirika hilo lilisema jeshi la Israel halikutoa kauli kuhusu madai mahsusi yaliyotolewa. Hata hivyo, msemaji mmoja alisema wafungwa "hushughulikiwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa."

Msemaji huyo aliongeza kwamba vikosi vya kijeshi vya Israel "havijawahi, na havitawahi, kuwalenga waandishi wa habari kimakusudi," na kwamba ukiukaji wowote wa itifaki "utachunguzwa." Idara ya magereza ya Israel, ambayo pia iliwasiliana na CPJ kuhusu madai hayo, ilisema kwamba kwa ufahamu wake "hakuna matukio kama hayo yaliyotokea."

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii