Zaidi ya watu 400 wameuawa tangu kundi la waasi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda lilipozidisha mashambulizi katika jimbo la Kivu Kusini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Idadi hiyo imetolewa na utawala wa Kivu Kusini ambao pia umeeleza juu ya uwepo wa vikosi maalum vya usalama vya Rwanda katika mji wa Uvira.
Kwa mujibu wa msemaji wa serikali ya Kivu Kusini, wengi waliouawa katika maeneo ya Uvira na Bukavu ni wanawake, watoto na vijana wadogo.
Taarifa iliyotolewa na serikali ya Kivu Kusini imeongeza kuwa, vikosi vilivyopo mjini Uvira vinajumuisha wanajeshi maalum wa Rwanda na baadhi ya mamluki wao wa kigeni.
Mashambulizi ya hivi karibu ya waasi wa M23 yametokea licha ya makubaliano ya amani yaliyosimamiwa na Marekani na kusainiwa wiki iliyopita na marais wa Kongo Felix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame mjini Washington.