Mapigano kati ya Thailand na Cambodia yaanza tena

Thailand imedai leo Jumatatu kutumia ndege "kushambulia malengo ya kijeshi" na "kuzuia mashambulizi ya Cambodia," baada ya mmoja wa wanajeshi wake kuuawa mpakani. Hii imeongeza mvutano, kwani makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya nchi hizo mbili yalisitishwa mnamo mwezi Novemba.

Mwanajeshi wa Thailand ameuawa na wengine wanne kujeruhiwa katika mapigano kwenye mpaka na Cambodia, jeshi la Thailand limetangaza leo Jumatatu, Desemba 8, huku pande zote mbili zikilaumiana kwa mapigano hayo.

Vikosi vya Cambodia vimeshambulia jeshi la Thailand katika mkoa wa Ubon Ratchathani, "na kumuua mwanajeshi mmoja na kujeruhi wanne," msemaji wa jeshi la Thailand Winthai Suvaree amesema katika taarifa.

Kwa upande wake, Wizara ya Ulinzi ya Cambodia imesema kwamba vikosi vya Thailand vimezindua mashambulizi katika majimbo ya mpakani ya Preah Vihear na Oddar Meanchey mapema leo Jumatatu asubuhi, ikidai kwamba cambodia haikulipiza kisasi.

Thailand inatumia ndege "kushambulia malengo ya kijeshi" na "kuzuia mashamulizi ya Cambodia," jeshi la Thai limesema.

Watu 35,000 wahamishwa

Mamlaka katika jimbo la Oddar Meanchey la Cambodia limeripoti kwamba milio ya risasi ilisikika karibu na mahekalu ya Tamone Thom na Ta Krabei ya karne nyingi, na kwamba wanakijiji wametoroka makazi yao "kwa kuhodia usalama wao."

Wakati huo huo, jeshi la Thailand limesema kwamba takriban watu 35,000 wamehamishwa kutoka maeneo ya mpaka na Cambodia usiku wa kuamkia leo Jumatatu.

Majirani hao wawili wa Kusini-mashariki mwa Asia wana mzozo wa muda mrefu kuhusu utengano wa sehemu za mpaka wao wa kilomita 800 (maili 500), uliowekwa wakati wa enzi ya ukoloni wa Ufaransa. Maeneo yanayozozaniwa yana mahekalu kadhaa.

Mnamo mwezi Julai, siku tano za uhasama kati ya Thailand na Cambodia uligharimu mais ya watu 43 na kusababisha watu 300,000 kutoroka makaazi yao, kabla ya mpango wa amani uliosainiwa kwa pamoja mwishoni mwa Oktoba na Rais wa Marekani Donald Trump kupunguza mvutano.

Makubaliano hayo yalijumuisha kuachiliwa kwa wafungwa 18 wa Cambodia waliokuwa wakishikiliwa nchini Thailand kwa miezi kadhaa. Pande zote mbili pia zilikubaliana kuondoa silaha nzito na kuondoa mabomu kutoka maeneo ya mpaka.

Thailand ilisitisha utekelezaji wa makubaliano hayo mwezi Novemba, ikisema kwamba bomu la ardhini lililotegwa hivi karibuni liliwajeruhi wanajeshi wake wanne.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii