Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi ameongoza Menejimenti ya Wizara kumuaga Kamishna wa Polisi (CP) Benedict Wakulyamba ambaye aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Uhifadhi, baada ya kustaafu Utumishi wa Umma.
Akizungumza katika hafla hiyo Dkt. Abbasi amempongeza CP. Wakulyamba kwa utendaji uliotukuka uadilifu na uzalendo aliouonesha kipindi cha utumishi wake Wizarani hususan katika kuimarisha Sekta ya uhifadhi na kuhamasisha utalii nchini.
“Tumeshuhudia mchango mkubwa wa CP. Wakulyamba katika kuimarisha mifumo ya uhifadhi sambamba na juhudi zake katika kukuza utalii wa ndani na nje ya nchi, tunakushukuru kwa kazi nzuri uliyoifanya,” alisema Dkt. Abbasi.
Hata hivyo CP. Benedict Wakulyamba alieapishwa rasmi kuwa Naibu Katibu Mkuu tarehe 18 Juni 2023 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameitumikia vyema Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kujituma uaminifu na uhodari mkubwa hadi anapostaafu rasmi Utumishi wa Umma.