Wizara ya Kilimo imekabidhi vifaa vya umwagiliaji kwa wakulima 383 wa Wilaya za Songea na Nyasa mkoani Ruvuma vitakavyowasaidia kumwagilia zaidi ya ekari 500 za kilimo.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Zana za Kilimo na Umwagiliaji, Mhandisi Athuman Kilundumya, amesema Wilaya ya Songea imepata jozi 9 za mitambo zitakazonufaisha wakulima 116, huku Wilaya ya Nyasa ikipokea jozi 25 zitakazonufaisha wakulima 267.
Vifaa hivyo vinatokana na utekelezaji wa Programu ya Mifumo Himilivu ya Chakula nchini (Tanzania Food Systems Resilience Program - TFSRP) inayolenga kuimarisha mifumo ya uzalishaji wa chakula kwa kuhimiza matumizi ya teknolojia na mbinu bora zinazohimili mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kuongeza uwekezaji katika Sekta ya Kilimo.
Mha. Kilindumya amesema hayo wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa hivyo Oktoba 27 mwaka huu katika kijiji cha Marungu, Wilaya ya Nyasa na kubainisha kuwa wakulima wamegawanywa katika makundi ya watu 10 na kila kundi limepatiwa vifaa vya umwagiliaji ambapo Kila kundi lina uwezo wa kumwagilia ekari 10 kwa siku, hatua itakayoongeza uzalishaji na kuhakikisha upatikanaji wa mazao kwa wingi na kwa wakati.
Aidha amesema Serikali inaendelea kutekeleza miradi zaidi ya 700 ya umwagiliaji nchi nzima, ikiwemo miradi ya dharura katika mito midogo kwa lengo la kuhakikisha Tanzania inakuwa na kilimo cha umwagiliaji cha uhakika kinachopunguza utegemezi wa mvua.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas amewataka wakulima wanufaika kutunza vifaa hivyo kwa uangalifu mkubwa na kuongeza tija ya uzalishaji. Pia amezitaka Halmashauri kushirikiana na vikundi vya wakulima na kuanzisha vikundi vipya katika vijiji vyenye fursa za kilimo cha umwagiliaji.
Nao wakulima walioshiriki hafla hiyo wameishukuru Wizara ya Kilimo kwa kuwapelekea mitambo ya umwagiliaji, wakisema itawawezesha kulima bustani za vitunguu, nyanya na mbogamboga kwa urahisi zaidi.