Mkuu wa Wilaya ya Babati Mhe. Emmanuela Mtatifikolo Kaganda Oktoba 28 mwaka huu amekabidhi rasmi hundi za malipo ya fidia kwa kaya 28 za wakazi wa Bonde la Maisaka, waliopisha ujenzi wa mradi mkubwa wa chanzo cha maji. Jumla ya shilingi bilioni 2.9 zimetolewa kama fidia kwa wananchi hao katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa ofisi ya BAWASA.
Akizungumza katika tukio hilo Mhe. Kaganda amewapongeza wananchi kwa ushirikiano waliouonesha katika kufanikisha hatua hiyo muhimu na kuwasihi kutumia fedha hizo kwa matumizi sahihi, yatakayosaidia familia zao kuepuka migogoro ya baadae. Pia amesisitiza kuwa Serikali imejipanga kuboresha zaidi miundombinu ya huduma za msingi, ikiwemo upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa Babati.
Aidha Mkuu wa Wilaya amewaelekeza wananchi hao kuhakikisha wanazingatia muda uliopangwa wa kuondoka kwenye eneo hilo, ili kutoa nafasi kwa utekelezaji wa mradi huo muhimu kwa ustawi wa jamii nzima ya Babati.