Wajumbe wa Kamati za Utafiti na Ubunifu ambayo ni Kamati Elekezi na Kamati ya Kiufundi wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi uwazi na ubunifu ili kuhakikisha kuwa tafiti zinazofanyika zinatoa mapendekezo yanayotekelezeka.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Bi. Jenifa Christian Omolo wakati akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Dkt. Natu El-Maamry Mwamba katika uzinduzi rasmi wa Kamati za Utafiti na Ubunifu, Kamati Elekezi, na Kamati ya Kiufundi uliofanyika katika Ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma.
Bi. Omolo alieleza kuwa Wizara ya Fedha inatambua kuwa utafiti na ubunifu ni injini ya maendeleo endelevu na msingi wa mageuzi ya kisera, kiuchumi na kiutendaji.
Aidha alifafanua kuwa kuanzishwa kwa Kamati Elekezi na Kamati ya Kiufundi ni sehemu ya utekelezaji wa Mwongozo wa Utafiti na Ubunifu wa Wizara ya Fedha (2025), ambao umeweka mfumo rasmi wa kuratibu shughuli hizo ndani ya Wizara.
“Kupitia utafiti na ubunifu, Wizara inaweza kubaini changamoto, kuibua fursa mpya na kubuni suluhisho endelevu katika maeneo ya sera, bajeti, ukusanyaji mapato, matumizi ya fedha za umma na usimamizi wa uchumi kwa ujumla,” alisema Bi. Omolo.
Akielezea majukumu ya kamati hizo Bi. Omolo alisema kuwa Kamati Elekezi itakuwa na jukumu la kuchambua mawazo ya utafiti na ubunifu kupitia taarifa za tafiti na kupendekeza motisha kwa wabunifu pia kusimamia ubora wa utekelezaji wa tafiti hizo.
“Uteuzi wenu umezingatia uzoefu, weledi na uwezo wenu kiutendaji katika taasisi/idara mnazozitumikia.” aliongeza Bi. Jenifa
Kwa upande mwingine, Kamati ya Kiufundi itakuwa na jukumu la kuchambua mawazo ya tafiti na bunifu, kuhakikisha ubora na uzingatiaji wa maadili ya utafiti, pamoja na kuwasilisha taarifa za utekelezaji kwa Kamati Elekezi kwa ajili ya hatua zaidi.
Kwa niaba ya wajumbe wa kamati hizo Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mipango katika Wizara ya Fedha, Bw. Alex Mwakisu, aliahidi kuwa watafanya kazi kwa ushirikiano na kwa wakati ili kuhakikisha kuwa tafiti na bunifu zinazofanyika zinakuwa na mchango chanya kwa Serikali na Taifa kwa ujumla.