Serikali inaendelea na zoezi la uthamini maeneo yatakayopitiwa na ujenzi wa Mradi wa Reli ya Kisasa SGR kipande cha sita kutoka mikoa ya Tabora hadi Kigoma katika wilaya za Tabora Mjini, Uyui, Urambo, Kaliua, Uvinza pamoja na wilaya ya Kigoma.
Timu kutoka ofisi ya Mthamini Mkuu ikiongozwa na Mthamini Kiongozi FRV James Mwanakatwe ipo mkoani Kigoma ikiendelea na kazi ya uhamasishaji pamoja na ukusanyaji taarifa za mali uwandani kwa wananchi ambao maeneo yao yanaguswa na mradi huo.
Akizungumza wakati wa utoaji elimu katika zoezi la uthamini uwandani Oktoba 27 mwaka huu wilayani Kigoma FRV Mwanakatwe ameeleza kuwa, Ofisi ya Mthamini Mkuu imepewa jukumu na serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) kufanya uthamini wa fidia kwa kipande cha pili hadi sita ambapo kwa sasa wako kipande cha sita.
Kwa mujibu wa FRV Mwanakatwe timu hiyo inaendelea kwa kasi na imeshafanya uthamini wa vipande 52 vya ardhi ikiwemo kipande cha daraja la mto Malagarasi lenye urefu km 3 ambalo liko katika hatua za mwisho za utekelezaji.
Amesema zoezi linaloendelea vizuri na kwa sasa wanaendelea na uthamini wa kilomita 72 hususan kwenye maeneo ambayo ni vipaumbele vya mkandarasi na kuweka wazi kuwa kazi hiyo ina takriban vipande 44.
"Kazi hii ni kilomita 72 na vipande vya ardhi takriban 44 ambavyo tutavifanyia kazi na tumeanza kazi rasmi hapa na kazi inafanyika kwa kasi ili kukamilisha zoezi hili kama ilivyopangwa" amesema Mwanakatwe.
Mthamini Mwanakatwe amesema katika Mradi wa SGR kipande cha 6 wameshafanya utafiti wa viwango vya fidia pamoja na kutoa elimu kwa wananchi wanaopitiwa na mradi huo ili wafahamu na kuzingitia masuala yanayohusu fidia.
Aidha amebainisha kuwa uthamini wa fidia kwa sasa unaendelea kwa kasi na timu ya Mthamini Mkuu itaendelea na jukumu lake la uthamini kwa umakini na uweledi mkubwa ili kufanikisha kazi hiyo kwa wakati.
Mkazi wa Nyamoli wilayani Kigoma ambaye eneo lake linapitiwa na mradi wa SGR Bw. Petrick Mathias amesema wameupokea mradi huo kwa furaha kubwa na kueleza kuwa, ni imani yao wanaopitiwa na mradi huo watalipwa fidia kwa viwango stahili.