Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo amewahimiza Watanzania kutumia ipasavyo fursa ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu kwa kulinda na kuendeleza amani ya nchi kwani ni nguzo muhimu ya maendeleo na ustawi wa taifa.
Prof. Mkumbo ametoa rai hiyo Oktoba 27 mwaka huu wakati akifungua Kongamano la Amani la Kitaifa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025, lililofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam. Prof. Mkumbo alifungua kongamano hilo kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango.
Kongamano hilo lililoandaliwa na Kamati ya Amani ya Kitaifa chini ya uratibu wa viongozi wa dini nchini linalenga kuhamasisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
Dhamira kuu ni kuhakikisha kuwa amani na utulivu vinatawala katika kipindi chote cha uchaguzi na vinaendelea kudumishwa hata baada ya uchaguzi.
Waziri Mkumbo amesema kuwa ingawa uchaguzi wa mwaka 2025 ni wa 14 tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini na wa 7 katika kipindi hiki cha mfumo huo, Tanzania haijawahi kuvuruga amani na utulivu.
Hivyo ameongeza kuwa licha ya changamoto zinazojitokeza, ni jukumu la kila Mtanzania kuhakikisha umoja, mshikamano, na utulivu vinaendelea kudumishwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
“Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu unatukumbusha mambo muhimu tunayopaswa kuyatunza, ikiwemo utu, haki, usawa, upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa, demokrasia, muungano na amani,” alibainisha Prof. Mkumbo.
Aidha Waziri Mkumbo amewashukuru viongozi wa dini kwa niaba ya Rais Samia, kwa kuandaa vyema shughuli za kuombea amani nchini na kuendesha makongamano ya kuhamasisha mshikamano wa kitaifa katika mikoa ya Mwanza, Kilimanjaro, Mbeya, Lindi, Tabora, na Dodoma, akisema kuwa jitihada hizo zimechangia kuhifadhi amani na utulivu katika kipindi chote kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.