RAIS wa Marekani Donald Trump ametishia kuchukua hatua kali dhidi ya Rais wa Urusi Vladimir Putin endapo hatokubaliana kumaliza vita vinavyoendelea nchini Ukraine.
Trump amesema Putin anapaswa kujiandaa kwa maamuzi yoyote yatakayochukuliwa dhidi yake iwapo hatofikia makubaliano ya kusitisha mapigano hayo.
Ameeleza kuwa kuna uwezekano wa kuwakutanisha Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, na Putin, mara baada ya mazungumzo yanayotarajiwa kufanyika Alaska.
Hata hivyo, Trump amesema anasubiri matokeo ya mazungumzo yake na Putin, akionya kuwa huenda kusiwe na kikao kingine kati yao endapo hakutakuwa na muafaka.
Rais huyo wa Marekani anatarajiwa kukutana na Putin huko Alaska, kwa lengo la kutafuta suluhu ya vita vya Urusi na Ukraine ambavyo vimeendelea kwa takriban miaka mitatu na nusu.