Aliyekuwa Waziri wa Sheria wa Kongo kutumikia miaka 10 jera

Kesi iliyoanza mwezi mmoja uliopita dhidi ya aliyekuwa Waziri wa Sheria wa Kongo Constant Mutamba, anayetuhumiwa kujaribu kutakatisha karibu dola milioni 20, imefungwa siku ya jana Jumatano, Agosti 13 mwaka huu kwa Mwendesha mashtaka kuomba miaka 10 ya kazi ya kulazimishwa. 

Mbali na miaka 10 ya kazi ya kulazimishwa, mwendesha mashtaka ameongeza muongo mwingine wa kutoshikilia wadhifa wowote rasmi baada ya kutumikia kifungo chake.

Wakati huohuo, upande wa utetezi unaamini kuwa hakuna uhalali wa kumtia hatiani Constant Mutamba, ukidai kuwa hakuna dola hata moja iliyofujwa kuhusiana na kandarasi yenye utata ya ujenzi gereza huko Kisangani, kaskazini mashariki mwa DRC.

 Kwa upande wake Mutamba, amebainisha kwamba taratibu za kisheria zimekuwa na lengo moja tu ambalo ni la kumwondoa serikalini. Uamuzi wa Mahakama Kuu utatolewa baada ya wiki mbili, tarehe 27 Agosti.

Kesi hiyo inatokana na mipango ya kujenga gereza huko Kisangani, mji mkuu wa mkoa wa Tshopo kaskazini-mashariki, ambayo ilikuwa eneo la vita vya siku sita kati ya majeshi ya Rwanda na Uganda mnamo Juni 2000. Gharama ya jumla ya mradi huo ni dola milioni 39. Mnamo Aprili 16, kiasi cha dola milioni 19.9 kilihamishwa kwa agizo la Mutamba kutoka kwenye akaunti ya Hazina ya Kulipa waathiriwa wa Shughuli Haramu za Uganda nchini DRC (FRIVAO) hadi akaunti ambayo sio ile iliyotajwa katika mkataba kati ya Wizara ya Sheria na Sayuni Construction SARL iliyotiwa saini siku mbili kabla.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii